April 14, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mwenyekiti wa Chadema ashitakiwa kwa Uhaini

Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema

TUNDU Lissu, mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akituhumiwa kwa uhaini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mwenyekiti wa taifa wa Chadema, anadaiwa kuchochea uasi nchini. Amesomewa shitaka hilo na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, Nassoro Katuga.

Lissu anatetewa kwa sasa na mawakili sita wa kujitegemea – Dk. Rugemeleza Nshalla, Dickson Matata, Jebra Kambole, Michael Lugina, Hekima Mwasipu na Gaston Garubindi.

Mapema jeshi la Polisi nchini lilisema lilimkamata Lissu jana mkoani Ruvuma kwa tuhuma za uchochezi wa kutishia kutofanyika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa Oktoba mwaka huu.

Katika taarifa yake, jeshi hilo, limetoa onyo kwa vyama vyote vya siasa kutotoa maneno ya uchochezi, kashfa kwa polisi au serikali ama kuanzisha viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Haya yanajiri siku moja baada ya keshi hilo, kuwashambulia kwa mabomu ya machozi wafuasi wa Chdeama na kuwazuia viongozi wao wakuu, kuendelea na mikutano yao na kuzungumza na waandishi wa habari mjini Songea.

Lissu alikamatwa jana Jumatano, baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara mkoani Ruvuma, katika ziara yake ya kunadi msimamo wa chama hicho wa ‘No Reforms, No Election (Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi.”

No Reforms, No Election, ni msimamo wa kisera wa chama hicho uliopitishwa na vikao vya juu vya Chadema, kuanzia Kamati Kuu ya tarehe 2 na 3 Desemba 2024.

Kamati Kuu iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe, ilisisitiza kuwa haitoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu kama hakutafanyika mabadiliko ya kimfumo katika uchaguzi, ikiwa ni pamoja na marekebisho ya katiba, sheria na kuhakikisha kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Aidha, Lissu na chama chake wamekuwa wakieleza kuwa uchaguzi huo, hautafanyika iwapo madai hayo hayatafanyika.

About The Author

error: Content is protected !!