
KAMPUNI ya Marvel Gold kutoka nchini Australia imefika nchini kujitambulisha na kuelezea mpango wao wa kuanzisha mgodi mkubwa wa dhahabu katika Wilaya ya Hanang’ Mkoa wa Manyara. Anaripoti Apaikunda Mosha, Manyara … (endelea).
Waziri wa Madini Anthony Mavunde leo Aprili 9, 2025 amefanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Timothy Strong, juu ya uwekezaji wa kampuni hiyo kwenye sekta ya madini.
Awali, akizungumza katika kikao hicho, Mavunde amewapongeza wadau hao kwa kuichagua Tanzania kufanya uwekezaji wao na kuwahakikishia kwamba serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha miradi kama hiyo yenye dhamira ya kukuza sekta ya madini inafanikiwa.
“Ninapokea watu wengi sana wenye nia kama ya kwenu, asilimia kubwa si wakweli kutekeleza mipango yao na wamekuwa na maneno mengi kuliko vitendo,” amesema Waziri Mavunde.
Ameongeza kwamba ana amini kwamba Kampuni hiyo itafanya kazi kubwa ya utafiti ili kama nchi ifanikiwe kupata mradi mwingine mkubwa wa uchimbaji madini ya dhahabu Mkoani Manyara.
Kwa upande wa mwekezaji huyo amesema kuwa “Tumeichagua Tanzania kwasababu ni nchi ambayo ina amani na usalama na mazingira mazuri ya uwekezaji,na tumevutiwa na mpango mzuri wa Rais Samia Suluhu Hassan kuvutia uwekezaji nchini Tanzania.”
Ameeleza kuwa kampuni hiyo inategemea kuanza zoezi la utafiti wa kina ifikapo mwezi Septemba 2025, hivyo itafanya utafiti wa kina kwa kurusha ndege na baadaye kukamilisha hatua zote za utafiti wa madini.
ZINAZOFANANA
Watanzania wahimiza kufanya mazoezi kwa Afya
Waziri Masauni aelezea mafanikio ya Muungano
Ofisi ya Msajili Hazina yaendesha mafunzo kwa kamati za bunge