
HATIMAYE Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) imewarejesha madarakani aliyekuwa mwenyekiti wake Deodatus Balile na Bakari Machumu kuwa Makamu Mwenyekiti. Anaripoti Salehe Mohamed, Songea … (endelea).
Wawili hao walichaguliwa bila kupingwa katika uchaguzi uliofanyika leo, tarehe 4 Aprili 2025 mjini Songea mkoani Ruvuma.
Balile na Machumu sasa wataongoza TEF kwa miaka minne baada ya kutojitokeza kwa wanachama wengine kuwania nafasi hizo.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Frank Sanga amesema kwa mujibu wa katiba ya jukwaa hilo ibara ya 7 na 8 zinaeleza kama mgombea atakuwa mmoja na hakutakuwa na pingamizi atatangazwa mshindi.
Sanga amesema kuwa uchaguzi huo umezingatia matakwa ya katiba na kanuni za jukwaa hilo na wameufanya kwa uwazi ili jamii ione wahariri wanavyochagua bila kificho.
“Kamati ya Uchaguzi tulikuwa tumejiandaa vizuri na tulikuwa tumetengeneza karatasi za kupigia kura lakini wagombea kwa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti hawakuwa na pingamizi wala wagombea wengine.
“Hivyo kwa kutumia kifungu cha kanuni namba 8 na 9 iwapo mgombea atakuwa mmoja na hana pingamizi basi atatangazwa kuwa mshindi.Hivyo tunamtangaza Deodatus Mutalemwa Balile kuwa Mwenyekiti wa TEF na Bakari Machumu kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kutumia kanuni ile ile.”
Wakati Balile akitangazwa kuwa Mwenyekiti wa jukwaa hilo wahariri walilipuka kwa shangwe kuonesha kufurahishwa na ushindi wake na wakati akiomba kura Balile alisisitiza iwapo atashinda atashirikiana na kamati ya utendaji ya jukwaa hilo pamoja na wanachama wa jukwaa hilo kuendelea kujenga misingi ya taaluma ya habari lakini pia kuwa na jukwaa kuwa na uwezo kiuchumi na kuweza kujitegemea
Naye Makamu Mwenyekiti Machumu ameahidi kuutumia muda wake kutoa ushauri utakamuwezesha Mwenyekiti na kamati ya utendaji kuhakikisha jukwaa hilo linatimiza majukumu yake huku akisisitiza kuwa atahakikisha anasimamia mabadiliko ya kiuchumi kwa vyombo vya habari kwa kujikita katika teknolojia ya habari kwa digitali.
Uchaguzi huo pia ulishuhudia wajumbe watano kati ya 12 waliokuwa wakiwania ujumbe wa kamati tendaji (KUT) kuangukia poa.
Walioshindwa ni Peter Nyanje, Angela Akilimali, Miruko Simon, Yasin Sadiq na Ester Zelamula.
Walioshinda kwenye ujumbe wa kamati tendaji ni Bakari Kimwanga, Tausi Mbowe, Joseph Kulangwa, Salim Said Salim, Anna Mwasyoke na Jane Mihanji.
ZINAZOFANANA
STAMICO kuendeleza leseni za uchimbaji dhahabu Kigosi
Rais Samia azindua Mahakama kubwa zaidi Barani Afrika jijini Dodoma
Mfumo wa ukataji wa tiketi SGR warejea kama kawaida