
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Venance Mwasse, amebainisha kuwa shirika hilo lipo katika hatua nzuri ya kuendeleza leseni nane linazozimiliki katika Hifadhi ya Pori la Kigosi Mkoani Geita ambalo hivi karibuni limeruhusiwa kufanya shughuli za uchimbaji wa madini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).
Amebainisha hayo alipotembelea eneo hilo leo tarehe 4 Aprili, 2025 hivyo amesema kuwa STAMICO itaendelea kutekeleza jukumu lake la ulezi na uwezeshaji kwa wachimbaji wadogo.
Amesema kuwa Shirika lina mpango wa kupeleka mtambo mdogo wa uchorongaji eneo la Kigosi ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kwenye shughuli za utafiti kwa gharama nafuu, aidha amewataka wachimbaji hao wadogo kutovamia leseni za Shirika zilizopo eneo hilo kwani kwa kufanya hivyo kutafifisha juhudi za kuwahudumia.
Mwasse alibainisha kwamba ili kuwawezesha zaidi wachimbaji wadogo, Shirika lipo tayari kuwapa taarifa za utafiti wa maeneo ambayo kwa sasa wanayamilki kihalali ndani ya hifadhi hiyo ambayo hapo awali yalikua chini ya umiliki wa STAMICO.
Katika hatua nyingine, Mwasse alitoa wito kwa wachimbaji wadogo kujikita kufanya uchimbaji salama ndani ya maeneo au vitalu vyao walivyogawiwa na Tume ya Madini hivi karibuni na kuacha kufanya uvamizi katika maeneo yenye leseni za STAMICO.
Mwasse pia alitembelea mtambo wa kuchenjua na kuchakata dhahabu unaomilikiwa na Kampuni ya NGM uliopo Ushirombo Mkoani Geita katika ziara hiyo aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Mbogwe Jeremiah Hango, Afisa Tawala Wilaya ya Bukombe Limbe Ndaki na Mwakilishi Mhifadhi Mkuu Pori la Kigosi Peter Edson Kibona pamoja na Mjiolojia Mkuu wa Shirika Alex Rutagwelela na Mhandisi Uchenjuaji Tiberio Kaduma.
ZINAZOFANANA
TEF yawarejesha tena Balile, Machumu
Rais Samia azindua Mahakama kubwa zaidi Barani Afrika jijini Dodoma
Mfumo wa ukataji wa tiketi SGR warejea kama kawaida