April 18, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Nchimbi: Chadema wasilazimishwe kushiriki uchaguzi 2025

Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi

 

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Mchimbi, amewataka Watazania wasiwalazimishe wanachama na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Anaripoti Salehe Mohamed, Songea … (endelea).

Dk. Nchimbi, ametoa kauli hiyo leo mkoani Ruvuma wakati akifungu Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ambao amesema Katiba inatoa haki ya mtu kupiga na kupigiwa kura.

Kiongozi huyo wa chama tawala anatoa kauli hiyo, kutokana na msimamo wa Chadema ambao wameweka wazi kuwa Hakuna Mabadiliko, ‘Hakuna Uchaguzi’ (No Reform, No Election’.

Chadema wanawahamasisha Watanzania wasishiriki uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyila Oktoba mwaka huu, kwa kile wanachodai sheria na kanuni hazitoi fursa sawa (zinaminya upinzani).

Akizungumzia msimamo wa Chadema, Dk Nchimbi amesema hakuna sababu ya kuwasaka wapinzani hao kwa kuwa wana uhuru na haki ya kususia au kushiriki uchaguzi.

Amesema nchi yetu ina utaratibu wa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi wa kutokuwapo kwa uchaguzi mwaka huu.

“Hakuna raia anayeweza kusema kuwa uchaguzi hautafanyika kwa kuwa hili ni takwa la kikatiba. Uchaguzi wa mwaka 2025 utafanyika kama ulivyopangwa,” amesema.

Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema

Dk Nchimbi amesema kuwa hata Rais Samia Suluhu Hassan, hana uwezo wa kuzuia uchaguzi usifanyike kwa kuwa hilo ni takwa la kikatiba ambayo ameapa kuilinda na kuitetea.

Amesema pamoja na haki ya raia kugombea pia hakuna haki ya kulazimisha chama chochote cha siasa kisiingie kwenye uchaguzi.

“Uchaguzi huu si wa mwisho maana kuna mingine. Chadema wanaweza kutoshiriki wa mwaka huu, mwingine wanaweza kuja kushiriki. Ni haki yao,” amesema

“Tusiwalazimishe Chadema kushiriki kwenye uchaguzi, wana haki ya kufanya wanachotaka. Si sahihi kuwalazimisha waingie kwenye uchaguzi maana wanayo haki ya kuamua wanachotaka ilimradi hawavunji sheria na Katiba ya nchi,” amesema

Dk Nchimbi ameongeza kuwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania uchaguzi utafanyika hata kama utahusisha chama kimoja ambapo wagombea wake watapigiwa kura za ndiyo au hapana.

“Nawaomba Chadema wanapokataa kupigiwa kura wasipoteze haki ya kwenda kupiga kura na watupigie sisi, namsihi ndugu yangu Tundu Lissu na wenzake wasipoteze haki zote mbili (kupiga na kupigiwa kura),” amesisitiza Dk. Nchimbi.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema wataendelea kutoa fursa sawa kwa Watanzania wote bila upendeleo ili kuboresha maendeleo ya taifa.

“Sisi tutawapa haki sawa hata wale wanaosusia watatumia haki yao vizuri na wale wanaoshiriki wasikwazwe” amesema

Katika hatua nyingine Dk. Nchimbi amesema CCm wataingiza ibara ya kuimarisha uchumi wa vyombo vya habari kwenye ilani ya CCM itakayokuja.

Amewataka wahariri wakemee wanasiasa wanaotamka mambo ya kuhatarisha amani, vurugu au kusababisha taifa livunjike.

“Kuna vitu vingine ambavyo wanasiasa wanavisema hovyo ni vema visiandikwe maana ninyi wahariri mna dhima kubwa kwa taifa” amesema.

About The Author

error: Content is protected !!