April 4, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Waziri Tabia ajilipua

Waziri wa Zanzibar, Tabia Maulid Mwita

 

WAZIRI wa Habari Zanzibar, Tabia Maulid Mwita ameahidi sheria mpya ya huduma za habari itakuwa tayari wakati wowote. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Akizungumza mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla, kwenye ufunguzi wa mkutano wa Maafisa Habari Serikalini, Waziri Tabia alisema ataiwasilisha sheria hiyo katika kikao cha Baraza la Mapinduzi [BLM], kilichotarajiwa kufanyika baadaye leo Alhamisi.

“Tutaisoma kwenye kikao cha BLM baadaye leo na tutaipeleka Baraza la Wawakilishi ambako natarajio ni kutungwa sheria mpya ikayowezesha kusimamia vema masuala ya habari na maafisa wetu wa habari,” alisema.

Kikao cha BLM hufanyika chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa BLM ambaye kwa sasa ndiye pia Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi [CCM]. Mara kadhaa Waziri Tabia amewahakikishia waandishi na wadau wa haki za binadamu kuwa maandalizi ya kupatikana sheria mpya ya huduma za habari yamefikia asilimia 80.

Mahitaji ya kuwepo Sheria ya Huduma za Habari iliyo rafiki Zanzibar yamekuwa kilio cha zaidi ya miaka 20 sasa kiasi cha wenyewe kuendelea kupigia mbiu jambo hilo baada ya kupeleka mapendekezo yao muda mrefu nyuma.

Ahadi ya sasa ya Waziri Tabia inaonesha kama vile Serikali imeamua kutimiza ahadi yake iliyoanza kutolewa na Rais Dk. Hussein Mwinyi, mbele ya hadhara ya kimataifa wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani mwaka 2023.

Tangu hapo, Kamati ya Ufuatiliaji Ustawi wa Habari ya Zanzibar [ZAMECO] inakazia mahitaji ya sheria mpya kwa kubainisha maeneo yanayoviza uhuru wa habari yaliyomo kwenye Sheria ya Uwakala wa Habari, Magazeti na Machapisho, Nam. 5 ya mwaka 1988 iliyorekebishwa miaka kadhaa baadaye lakini ikibakiza vifungu vya udhibiti na kuwaoa mamlaka makubwa Waziri wa Habari na hata Jeshi la Polisi ambako askari anaweza kukagua na kukamata vifaa.

“Tumemsikia kwa mara nyengine huyu Waziri Tabia. Tunamuomba sana ashike uongozi kwa Serikali kuondoa ukimya kuhusu suala hili kwa sababu ahadi zimekuwa nyingi,” amesema mjumbe mmojawapo wa Kamati hiyo leo.

Sheria mpya ya huduma za habari na ambayo itaendana na wakati wa sasa itawezesha kazi ya kutoa habari na taarifa mbalimbali kufanywa kwa uhuru na umakini zaidi kwani hakutakuwa na hofu kwa waandishi na wamiliki wa vyombo vya habari.

About The Author

error: Content is protected !!