April 4, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC yaingia makubaliano na TAFINA kuchochea ukuaji wa teknlojia utoaji huduma za fedha

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imesaini makubaliano ya ushirikiano na Umoja wa Makampuni yanayotoa Huduma za Kifedha kupitia Teknolojia Tanzania (TAFINA) ikiwa ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo kuongeza kasi ya ukuaji wa teknolojia katika utoaji wa huduma za kifedha sambamba na kuchochea uchumi jumuishi kupitia huduma za kifedha zilizorahisishwa kupitia teknolojia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo imefanyika mapema leo jijini Dar es Salaam ikihusisha wawakilishi kutoka taasisi hizo mbili. Mkurugenzi wa Biashara Benki ya NBC, Elvis Ndunguru na Mwenyekiti wa TAFINA, Cynthia Ponera waliziwakilisha taasisi hizo mbili kwenye makubaliano hayo yaliyosainiwa kwa mara ya kwanza baina ya TAFINA na taasisi ya kifedha nchini.

Akifafanua kuhusu makubaliano hayo, Ndunguru alisema pamoja na mambo mengine yanatoa fursa ya ushirikiano baina ya benki hiyo na makampuni yanayotoa huduma za kifedha kupitia Teknolojia nchini hatua ambayo kwa kiasi kikubwa itachochea kasi ya uboreshwaji wa mfumo wa malipo ya kidijitali na ujumuishi wa kifedha na uimarishaji wa uzingatiaji wa kanuni za kifedha miongoni mwa makampuni hayo.

“Kupitia makubaliano haya NBC tunakuwa kama walezi wa makampuni yanayofanya kazi za kibunifu kupitia teknolojia katika utoaji wa huduma za kifedha nchini. Ulezi wetu huu unahusisha pia utoaji wa suluhisho za kifedha kwa makampuni haya ikiwemo mikopo rafiki, kushirikiana nayo kwenye mikutano, mijadala ya sera, na matukio makubwa ya sekta ya fintech yanayoandaliwa na TAFINA,’’ alisema.

Kwa mujibu wa Ndunguru kupitia ushirikiano huo benki hiyo inathibitisha dhamira yake ya kuwa benki kinara katika sekta ya benki za kidijitali na ubunifu wa kifedha kuelekea mapinduzi makubwa ya utoaji wa huduma za kifedha.

“Kupitia ushirikiano huu, NBC na TAFINA tutashirikiana kuunda na kutoa bidhaa maalum kama vile njia za malipo kidijitali (payment gateways), mikopo ya kidijitali, na huduma za kifedha zilizounganishwa (embedded finance solutions). Ubunifu huu hautaimarisha kampuni za fintech pekee, bali pia utaongeza ujumuishi wa kifedha kwa Watanzania wote kwa kuhakikisha kuwa huduma za kifedha zinapatikana kwa urahisi, kwa gharama nafuu, na kwa ufanisi zaidi,” aliongeza.

Wakizungumza kuhusiana na hatua hiyo Katibu Mkuu wa TAFINA, Shadrack Kamenya na Meneja Mahusiano TAFINA, Julieth Kiluwa pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa ushirikiano huo walisema utawasaidia kwa kiasi kikubwa makampuni wanachama kupitia huduma mbalimbali za upendeleo kutoka benki hiyo ikiwemo mikopo rafiki itakayochochea ukuaji wa mitaji kwa wanachama hao pamoja na kupata fursa ya kuitumia benki hiyo kama mlezi kwenye shughuli zao mbalimbali za kiubunifu.

“Kupitia ushirikiano huu sasa tunashukuru kwa niaba ya wanachama wetu kuona kwamba tuna mshirika mwenye nguvu ambae anaweza kutushika mkono kuelekea ndoto zetu za kurahisisha utoaji wa huduma za kifedha kupitia teknolojia. Zaidi tunaimani kwamba kupitia mikopo ya NBC yenye upendeleo kwa wanachama wetu itasaidia ukuaji wa kampuni nyingi za kibinifu huku pia tukipata fursa ya kuwa na benki mlezi itakayokuwa karibu zaidi na sisi kwenye vumbuzi zetu zinazolenga kurahisisha utoaji wa huduma za kifedha kupitia teknolojia,’’ alisema.

About The Author

error: Content is protected !!