March 31, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali: Faida itokanayo na uwekezaji ifikie zaidi ya asilimia 10

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka

 

SERIKALI inataka faida itokanayo na uwekezaji ‘return on investment’ katika kampuni ambazo inaumiliki wa hisa chache iongezeke kutoka asilimia saba ya sasa hadi kufikia zaidi ya 10 mwaka ujao wa fedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea).

Dhamira hiyo ilielezwa Ijumaa, Machi 28, 2025, na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka wilayani Kibaha, mkoani Pwani, wakati wa kufunga mkutano wa siku tatu wa wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo serikali inaumiliki wa hisa chache.

“Niwape changamoto ya kukuza faida itokanayo na uwekezaji kutoka asilimia saba ya sasa kwenda zaidi ya asilimia 10 kwa mwaka. Na ili kufikia azma hii mnapaswa kuongeza ufanisi wa utendaji,” alisema.

Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia jumla ya taasisi 308 ambapo kati ya hizo 56 ni zile ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.

Jumla ya uwekezaji wa Sh. 86.3 trilioni umefanywa katika taasisi hizo, huku kati ya kiasi hicho Sh. 2.9 trilioni zikiwekezwa kwenye kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache na Sh. 83.4 trilioni kikienda kwa taasisi ambazo serikali ina umiliki wa asilimia 100.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka akizungumza na Wakurugenzi

Aidha, Balozi Kusiluka aliwapa changamoto wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo ina hisa chache kuongeza ufanisi gawio kwa serikali.

“Ninaamini mwaka ujao wa fedha nitaona gawio kutoka Taasisi mnazosimamia likiongezeka. Hiyo ni changamoto ninayowaachia,” alisema wakati wa mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Kwa mwaka wa fedha uliopita, serikali ilipata gawio la Sh195 bilioni kutoka kampuni zake ambazo ina umiliki wa hisa chache, kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Mafanikio yetu yataakisi juhudi za Serikali chini ya Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ambazo zimekuwa zikifanyika za kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya biashara,” alisema Dk. Kusiluka.

Alionesha imani yake kwa mwongozo ulioboreshwa wa Wakurugenzi wa Bodi wa Hisa chache uliozinduliwa Jumatano wiki hii wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere.

“Nimeupitia kwa kina na nimeona umejaa miongozo mizuri itakayotusaidia kutekeleza majukumu yetu kwa weledi na kwa wakati,” alisema Dk. Kusiluka, huku akiipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kutengeneza Mwongozo huo.

Ni katika muktadha huo aliwaelekeza wakurugenzi wa bodi kuutumia kikamilifu ili kuongeza ufanisi katika maeneo yao.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amewataka wawakilishi wa serikali kwenye bodi za kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu akizungumza na Wakurugenzi

Aliwataka wawakilishi hao ambao ni wakurugenzi wa bodi kuzitendee haki nafasi walizopewa ili kuhakikisha kuwa serikali inanufaika na uwekezaji iliofanya kwenye kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache.

“Nyie ni jicho la serikali hivyo mnapaswa kutokuchukulia kiwepesi nafasi mlizopewa, vinginevyo mtakuwa hamuitendei haki serikali na watanzania wote kwa ujumla,” Mchechu aliwaambia wakurugenzi hao.

Aliongeza: “Lazima mjidhatiti na kama unaona hauko kwenye nafasi ya kufanya hivyo kutokana na kutokuwa na muda wa kutosha, ni vyema ukasema ili nafasi hiyo wapewe wengine.”

About The Author

error: Content is protected !!