
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dk. Prosper Mgaya
SERIKALI imejivunia hatua ya kukiwwezesha Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kukamilisha maandalizi ya utoaji wa mafunzo ya Urubani. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Majivuno hayo yanatokana na chuo kukamilisha matakwa ya kupata ithibati kutoka TCAA na hivyo mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza mwezi Mei 2025.
Katika kukiwezesha chuo hicho kuanza mafunzo hayo Serikali mpaka sasa imetoa jumla ya takribani bil.6.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo cha NIT, Dk. Prosper Mgaya, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa chuo hicho katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Ifahamike kuwa kama nchi tumekuwa tukitegemea kwa kiasi kikubwa kupelekea watanzania kupata mafunzo ya urubani nje ya nchi. Hivyo Serikali na watanzania kwa ujumla tumekuwa tukitumia fedha nyingi sana za kigeni kusomesha marubani nje ya nchi.
Dk. Mgaya amesema kuwa kwa kuanzisha mafunzo hayo hapa nchini kwenye NIT kutapunguza gharama ya mafunzo kwa takribani asilimia 50 – 60 ambazo watanzania wengi wanatumia kupata mafunzo hayo nje ya nchi. Kuanza kwa mafunzo haya hapa nchini kutaokoa fedha za kigeni ambazo zimekuwa zikitumika.
Aidha amesema kuwa kuanza kwa mafunzo hayo kutaongeza idadi ya marubani wazawa hivyo kutapunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi kwa marubani wa kigeni ambao gharama yake ni kubwa.
Ameeleza kuwa mafunzo ya urubani yanahitaji kuwa na wakufunzi na vifaa vya kufundishia vinavyokidhi vigezo vya kimataifa.
“Katika kuhakikisha chuo kinaanza mafunzo ya urubani Serikali imegharamia mafunzo ya wakufunzi watano ambao wamepata mafunzo haya nchini Afrika ya Kusini kwa Gharama ya bil. 1.5 ikiwa ni wastani wa Mil.300 kwa kila mkufunzi.
Vilevile amesema Serikali imenunua ndege mbili za mafunzo aina ya Cesna 172 zenye injini moja ambazo tayari zipo nchini kwaajili ya kuanza mafunzo hayo.
“Ndege hizi zina thamani bil 2.9 na serikali ipo katika taratibu za ununuzi wa ndege nyingine tatu ikiwa ndege moja ya injini mbili ambayo itawasili mwezi Oktoba 2025 ambayo ina thamani ya bilioni 5.9 na Ndege mbili za injini moja zitawasili mwaka 2026.
Pia amesema Serikali imetoa eneo lenye ukubwa wa Ekari 60 katika kiwanja cha KIA mahsusi kwaajili ya mafunzo hayo ambapo ujenzi wa miundombinu unaendelea.
Pamoja na hayo Dk. Mgaya amesema chuo hicho kinatekeleza mradi wa kujenga ujuzi kwa maendeleo na uingiliano wa kikanda katika Afrika Mashariki, ujulikanao kama “East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project (EASTRIP)”.
Amesema kupitia mradi huo, NIT itapokea Dola za Kimarekani Mil.21,250,000 sawa na Shillingi za Kitanzania bil.49 kwa ajili ya kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji (Center of Excellence in Aviation and Transport Operations – CoEATO).
“Kupitia Mradi huo Serikali imekiwezesha Chuo kujenga majengo Matano katika Kampasi ya Mabibo -Dar es salaam ambao ujenzi wake kwa ujumla umefikia asilimia 97.
“Ujenzi huu utakamilika ifikapo mwezi June 2025.Gharama ya ujenzi wa majengo haya ni bil.24.9 ambapo mradi huu umefadhili ujenzi wa jengo la mafunzo ya urubani katika eneo la KIA ambalo Serikali imetoa,” amesema Dk. Mgaya.
ZINAZOFANANA
Aweso aomba radhi watendaji wa Wizara ya Maji
Wanafunzi wahimizwa kulinda miundombinu ya shule
Asilimia 11 tu ya wanawake wamenufaika na TIB