
BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) ambae ni mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya NBC imekabidhi basi jipya kwa Klabu ya soka ya Coastal Union FC ya jijini Tanga inayoshiriki ligi hiyo ikiwa ni mwendelezo wa dhamira ya dhati ya benki hiyo katika kuboresha ligi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tanga … (endelea).
Coastal Union FC inakuwa klabu ya nne inayoshiriki ligi hiyo kunufaika na mpango huo unaohusisha mkopo nafuu kutoka benki ya NBC baada ya klabu za KMC ya Kinondoni, Singida Big Stars na Namungo FC kunufaika na mpango kama huo hapo awali. Mkopo wa basi la Coastal Union FC unaifanya benki ya NBC kuwa imetoa jumla ya mikopo yenye thamani ya Sh. 1.2 bilioni kwenye usafiri wa klabu hizo nne vilivyonufaika na mpango huo.
Hafla ya makabidhiano ya basi hilo iliyohusisha paredi maalum la basi hilo katika maeneo mbalimbali ya jiji la Tanga, imefanyika leo kwenye tawi la benki ya NBC jijini Tanga ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Stephan Sumaye aliemuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dk. Batilda Burian.
Pia hafla hiyo ilihusisha uwepo wa Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Al-Hajj Abdulrahman Shiloow, viongozi waaandamizi wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya NBC, Elvis Ndunguru, Mwenyekiti wa Klabu ya Coastal Union FC, Muhsin Ramadhan Hassan, mdhamini wa klabu hiyo kampuni ya RATCO Express, benchi la ufundi pamoja na wachezaji.
Akizungumza kwa niaba ya Balozi Dk. Burian, DC Sumaye pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa hatua hiyo muhimu, alisema hatua hiyo imekuja kipindi ambacho uongozi wa mkoa huo upo kwenye utekelezaji wa wito wa Rais Samia wa kuchochea kasi ya maendeleo mkoani humo ikiwemo sekta ya michezo kupitia uboreshaji wa miundombinu ya michezo.
“Kilichofanywa na NBC leo ni kama kuunga mkono muitikio wa wito huu wa Rais Samia. Nimevutiwa zaidi kuona NBC wanagusa hadi masuala ya bima kwa wanamichezo hilo ni jambo zuri zaidi. Ombi Langu kwa wachezaji na viongozi wa klabu ni kuhakikisha kwamba jitihada hizi zinatoa majibu kwenye matokeo ya uwanjani,’’ alisema.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo iliyoambatana na msafara maalum kutoka kwenye tawi la NBC hadi Makao makuu ya klabu hiyo, Ndunguru alisema basi hilo ni sehemu ya mpango wa utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vilabu vinavyoshiriki ligi hiyo.
“Ukosefu wa vyombo vya usafiri maalum kwa ajili ya timu zinazoshiriki ligi Kuu ya NBC imekua ni moja ya chanzo cha vikwazo vingi katika gharama za uendeshaji na utendaji wa timu husika.Jitihada zetu kama wadhamini haziishii hapa tu kwenye mikopo ya usafiri bali tunagusa maboresho ya baadhi ya viwanja vinavyotumia kwenye ligi hii, tunatoa bima za afya kwa wachezaji na mabenchi ya ufundi na zaidi tunatoa huduma za kifedha ikiwemo elimu ya kifedha kwa wadau wa michezo wakiwemo wachezaji,’’ alisema.
Wakizungumza kwenye hafla hiyo Mwenyekiti wa Klabu ya Coastal Union FC, Muhsin Ramadhan Hassan na Mstahiki Meya Al-Hajj Shiloow pamoja kuishukuru benki hiyo kwa jitihada zake za kuiboresha ligi hiyo walikiri kuwa klabu hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya usafiri bora hapo awali hali ambayo iliongeza changamoto katika ubora wat imu hiyo.
“Tanga sasa tumeweka alama kupitia benki ya NBC. Kupitia usafiri huu sasa tuna uhakika wa kusafirisha wachezaji wetu kwenda popote, wakati wowote tena wakiwa na utulivu zaidi. Ni wazi sasa tunakwenda kuongeza ushindani zaidi kwenye ligi kupitia hatua hii ya leo,’’ alisema Mwenyekiti Muhsin.
ZINAZOFANANA
Timu za kukupa pesa zipo Meridianbet leo
Reflectors zatolewa kwa bodaboda
ODDS KUBWA na machaguo zaidi ya 1,000 yapo hapa