
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso ameomba radhi kwa watendaji wa wizara ya maji na wote waliopoteza kazi kwa kuwa kuna wakati alikuwa mkali katika idara hiyo ili kuhakikisha wanafikia malengo. Anaripoti Apaikunda Mosha, Dr es Salaam … (endelea).
Akizungumza leo tarehe 22 Machi 2025 katika hafla ya kilele cha wiki ya maji iliyofanyika katika ukumbi wa mlimani city jijini Dar es salaam, Aweso amesema, Rais Samia mara nyingi amekuwa akisema haridhishwi na matokeo ya miradi ya maji wakati serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezwaji wa miradi hiyo.
“Nakumbuka siku moja nilienda Bukoba vijijini nilipofika walikuwa wanatupa hali ya utekelezaji wa miradi ya maji, katika zile taarifa waliniambia kuna visima wanavichimba ilivofika jioni nikawaambia naomba twende kwenye hivo visima, ..tulivoenda kukagua unamuuliza Mhandisi wa maji kisima kikowapi anakwambia Aki ya Mungu Waziri jana kilikuwa hapa!,” amesema Aweso.
Kwa mujibu wa Aweso baadhi ya watendaji wengi katika sekta hiyo walikuwa sio waaminifu na wawajibikaji kiwango cha kumfanya awe mkali, ameeleza kuwa wakati wa ziara ya mradi wa Njombe vijijini walikuwa wanaletewa fundi badala ya muhandisi wa maji na wao wakiwa hawana taarifa kamili ya miradi hiyo ambayo imewekezwa fedha nyingi.
Amesema pia katika mradi mwingine wa Shinyanga vijijini, zaidi ya Sh. 1.3 Bilioni zimetolewa katika eneo linaitwa Mwakitorio lakini wananchi hawapati maji na ukimuuliza Mhandisi wa maji anahusisha Imani za kishirikina kuwa zinakwamisha utekelezaji wa mradi huo.
“Unamwambia Mhandisi waeleze wananchi kwanini hawapati maji anakwambia Mheshimiwa Waziri sijawahi kuona wananchi wachawi kama katika hichi kijiji, namuuliza unasemaje, anasema Mheshimiwa hapa tumefanya kazi kubwa lakini usiku mabomba yanapaa kama kama ndege,” amesema Aweso.
Ameendelea kusema kuwa Miradi mingine ilikuwa niya gharama kubwa amabayo ilifanya wizara hiyo kushughulikia miradi hiyo wenyewe, ikiwa ni pamoja na mradi wa tanki la maji lenye lita laki 2 ambalo makadirio ya mkandarasi yalikuwa Sh. 5 bilioni badala yake ukajengwa kwa Sh.1.5 Bilioni.
Aidha, amesema Wizara ya maji imeona umuhimu wa kufanya mabadiliko katika sekta hiyo kutokana na madabiliko ya teknolojia hivyo sera hii ambayo inaenda kuzinduliwa imezingatia kutoa kipaumbele uwekezaji wa watu binafsi ili kuongeza ubora katika sekta hiyo.
ZINAZOFANANA
Wanafunzi wahimizwa kulinda miundombinu ya shule
NIT yajivunia uanzishwaji wa chuo cha marubani
Asilimia 11 tu ya wanawake wamenufaika na TIB