March 23, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Asilimia 11 tu ya wanawake wamenufaika na TIB

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo TIB, Lilian Mbassy

 

LICHA ya Benki ya Maendeleo (TIB) kuwekeza kiasi cha Sh. 630 bilioni kwa miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Siluhu Hassan kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia sekta mbalimbali bado wanawake hawana mwitikio mkubwa wa kuchangamkia fursa hiyo na mpaka sasa ni aailimia 11 tu walionufaika na TIB. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo TIB, Lilian Mbassy alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Benki hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.

Kutokana na hali hiyo ya akina mama kutotojitokeza kupata fursa za kifedha katika benki hiyo umeandaliwa mkakati kabambe wa kuhamasisha wanawake kuchangamkia fursa mbalimbali za kibiashara kupitia Benki hiyo.

Liliani amesema kuwa asilimia 11 ya wanawake ambao wananufaika na pesa za maendeleo kupitia Benki hiyo imebainika wapo wanaosimamia miradi ya maendeleo au kumiliki miradi hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji huyo ameeleza kuwa Benki ya Maendeleo (TIB) imewekeza zaidi ya Sh. 630.3 bilioni katika miradi ya maendeleo hadi kufikia Desemba 2024.

Ambapo kati ya kiasi hicho, Sh. 408.3 bilioni zipo kwenye mizania ya Benki,huku mifuko tisa inayosimamiwa na Benki ikichangia uwekezaji wa Sh. 222 bilioni.

Akifafanua juu ya uwekezaji huo amesema ni wa miradi ya muda wa miaka 5-15 katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Mbassy ameeleza kuwa uwekezaji huo umegusa maeneo ya kipaumbele ya Serikali pamoja na malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambapo bil.162.7 zimewekezwa kuongeza usalama wa chakula na kupunguza njaa.

Amesema kuwa Sh. 4.3 bililioni zimewekezwa kuboresha elimu kupitia miradi ya taasisi za elimu na Sh. 22.4 bilioni zimewekezwa katika upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira kupitia miradi ya mamlaka za maji.

“Uwekezaji mwengine ni Sh. 11.5 bilioni zimewekezwa katika nishati safi na nafuu kupitia mradi wa upanuzi wa nishati ya umeme vijijini (Tanzania Rural Electrification Expansion Programme-TREEP) na bil. 250.7 zimewekezwa katika ukuaji wa
uchumi na ajira, ikihusisha sekta za utalii, viwanda, na usafirishaji na Sh. 24.7 bilioni zimewekezwa kuboresha miji na makazi,” amesema Mbassy.

Aidha Mkurugenzi huyo amesema kuwa kupitia uwekezaji huo zaidi ya ajira mpya 12,547 zimezalishwa kutokana na Benki kufadhili miradi ya muda wa kati na mrefu nchini.

Akizungumzia mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya Benki hiyo, Mbassy amesema TIB kama benki ya maendeleo ni taasisi ya kisera ambayo ina jukumu la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kitaifa hususani kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo hivyo mwaka 2025,vipaumbele vyake vimejikita katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kitaifa ili kuongeza kasi ya maendeleo,pamoja na kutekeleza vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita.

Vilevile amesema kuwa Benki itaendelea kukuza mtaji wa Benki kwa kushirikiana na taasisi za fedha za kimataifa ili kupata mikopo ya riba nafuu kwaajili ya kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo yenye athari Chanya kwa jamii na uchumi.

About The Author

error: Content is protected !!