March 21, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Msimu wa Eid na Pasak: NBC yatoa punguzo la 20% kwa manunuzi

 

KUELEKEA Msimu wa Sikuku za Eid na Pasaka, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC ) imeingia makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya Hope Holding inayomiliki maduka ya Sketchers, Flormar, Bottega Verde, DeFacto na LC WaIKIKI yaliyopo kwenye jengo la Morocco Square jijini Dar es Salaam ili punguzo la 20% kwa wateja watakaofanya manunuzi kwenye maduka hayo na kulipia kwa kutumia kadi za benki hiyo.

Makubaliano hayo ni muendelezo wa mkakati wa benki NBC katika kuhamasisha utumiaji wa huduma za kibenki kwa njia za kidigitali katika ufanyaji wa miamala miongoni mwa wateja wake hususani kipindi hiki cha kuelekea katika msimu wa Sikukuu za Eid el Fitr na Pasaka.

Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika leo kwenye viunga vya jengo la Morocco Square jijini Dar es Salaam yakiwahusisha Mkuu wa Kitengo cha Miamala ya Kibenki kutoka Benki ya NBC, Mangire Kibanda na Meneja Masoko wa Kampuni ya Hope Holding, Micky Decha. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na maofisa wengine kutoka pande zote mbili.

Akizungumzia makubaliano hayo, Mangire alisema hatua hiyo ni muendelezo wa utamaduni wa benki hiyo katika kutoa fursa kwa wateja wa benki hiyo kufurahia kupitia punguzo la bei kwenye manunuzi ya huduma mbalimbali kuelekea katika vipindi vya sherehe mbalimbali za kitaifa zikiwemo sikukuu za kidini.

“Makubaliano yetu na wenzetu wa Hope Holding ni muendelezo wa jitihada za benki ya NBC tukilenga kutoa fursa kwa wateja wetu kufurahia miamala iliyorahisishwa wanapofanya manunuzi yao ya mavazi ya aina mbalimbali kwa ajili ya marafiki, familia, na wapendwa wao kuelekea kwenye sikukuu hizi za Eid el Fitr na Pasaka huku wakinufaika kupitia upendeleo wa bei kupitia punguzo la hadi asilimia 20 kwenye manunuzi kwenye maduka haya matano kwasasa yaliyopo hapa Morocco Square,’’ alisema.

Kwa upande wake, Decha pamoja na kuishukuru benki ya NBC kwa makubaliano hayo alisema punguzo hilo la asilimia 20 ni msaada mkubwa kwa wateja wao wanaomiliki kadi za benki ya NBC huku akionyesha kuvutiwa zaidi na jitihada za benki hiyo kuhamasisha matumizi ya kidigitali katika ufanyaji wa miamala kwa kuwa ni njia rahisi, salama zaidi kwa wateja na inawasaidia wao kama wafanyabiashara katika utunzaji wa kumbukumbu za malipo.

“Ushirikiano huu utakuwa na tija zaidi kuanzia kwa wateja wetu ambao kwasasa hawatalazimika kutembea na kiasi kikubwa cha fedha wanapokuja kufanya manunuzi na zaidi kwasasa wataweza kupata bidhaa zetu kwa punguzo la asilimia 20. Tunawakaribisha sana hususani kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu za Eid el Fitr na Pasaka,’’ alisema.

About The Author

error: Content is protected !!