
Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango
SERIKALI imezitaka Taasisi za Fedha nchini kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu bila kuwaumiza wananchi kwa kuhakikisha kuwa zinatoa huduma za kifedha kwa uwazi, haki na uwajibikaji. Anaripoti. Apaikunda Mosha, Mara … (endelea).
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Salum Mtelela alipokutana na Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo ipo mkoani Mara kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali.
“Serikali huweka kanuni na taratibu maalumu ili kulinda wateja na kuhakikisha kuwa taasisi hizi haziwadhulumu wananchi kupitia riba kubwa, ada zisizoeleweka au mikataba mibovu”, alisema Mtelela.
Aidha, Mtelela amezitaka Taasisi za Fedha kuepuka utoaji wa mikopo holela bila kuzingatia uwezo wa mkopaji kurejesha deni na kutumia njia za kisheria katika kudai madeni badala ya vitisho na manyanyaso.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Oscar Nchemwa, ameshauri Serikali kuhakikisha inadhibiti uanzishwaji holela wa Taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwa wananchi bila kufuata sheria.
Naye Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Glory Swai, ameishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwapatia mafunzo ya elimu ya fedha kwa watumishi wa Halmashauri hiyo.
Ameishauri Wizara ya Fedha ihakikishe elimu ya fedha inatolewa kwa makundi yote nchini, lakini pia itolewe kwa watoa huduma ili watoe huduma kwa kufuata kanuni na taratibu.
Akizungumzia zoezi la utoaji elimu ya fedha katika Mkoa wa Mara, Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Stanley Kibakaya, amesema kuwa wananchi wa mkoa huo wamejitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo muhimu kwa ustawi wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Amesema kuwa mafunzo ya elimu ya fedha mkoani humo, yalitolewa katika makundi mbalimbali ikiwemo wanafunzi, wajasiriamali, vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalumu.
Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Taasisi zake imemaliza zoezi la utoaji elimu ya fedha katika Mkoa wa Mara na timu ya wataalamu itaelekea Mkoa wa Mwanza ambao utakua mkoa wa 16 kufikiwa na elimu ya fedha kati ya mikoa 26 ya Tanzania.
ZINAZOFANANA
TAZARA sasa ipo chini ya usimamizi wa China
MSD yaokoa Sh. 15.8 bilioni
Wassira amchongea Mo Dewji kwa serikali kwa kutelekeza mashamba ya Rungwe