March 18, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mbibo ahimiza maadili kwa watumishi wa Wizara Madini

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo

 

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amewataka watendaji na watumishi wa Wizara ya Madini kuzingatia uadilifu na maadili katika utekelezaji wa majukumu yao. Anaripoti Apaikunda Mosha. Dodoma…(endelea). 

Ameyasema hayo leo 18 Machi  2025 wakati akifungua Kikao kazi cha Watumishi wa Wizara ya Madini ambapo amewataka watendaji na watumishi hao kuzingatia miongozo ya Serikali sambamba na kuepuka vitendo visivyo vya kimaadili kama kupokea rushwa.

Ameeleza kuwa watumishi hao wanapaswa kuepukana na vitendo hivo visivokuwa halali ili kuhakikisha Sekta ya Madini inakua na kuongeza tija pamoja na kukuza mchango wake katika Pato la Taifa (GDP) na maendeleo endelevu ya kiuchumi kwa ujumla.

Amesema kwamba rushwa ni adui mkubwa wa haki, pia ni kati ya makosa ya kimaadili na uadilifu na lengo watumishi  ni kuhakikisha kuwa wanatoa huduma bora kwa wateja wao na kuwa mfano bora wa utumishi wa umma.

Aidha, Mbibo amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuendelea kuzingatia masuala muhimu ya kiafya ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya mwili ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama shinikizo la damu, kisukari, maradhi ya moyo, afya ya akili na mengineyo sambamba na magonjwa ya kuambukizwa kama UKIMWI.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Madini Festus Mbwilo amesema kuwa lengo la kikao kazi hicho cha watumishi wa Wizara ni kuhakikisha ufanisi unaongezeka katika utekelezaji wa programu na majukumu ya Wizara ili kufikia malengo ya Wizara na Serikali kwa ujumla kupitia Sekta ya Madini.

About The Author

error: Content is protected !!