
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge, Justin Nyamoga
MWENYEKITI wa Kamati ya kudumu ya Bunge, Justin Nyamoga, ametoa wito kwa TAMISEMI kuhakikisha inafuatilia ukamilishwaji wa miundombinu ya maabara na vifaa vyake katika shule 26 maalum za Sayansi za wasichana zilizojengwa nchini. Anaripoti Apaikunda Mosha, Geita … (endelea).
Ameyasema hayo mapema leo 17 Machi 2025 wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua mradi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Geita, moja kati ya shule 26 za Kitaifa za Sayansi zilizojengwa hapa nchini.
“Tumetoa muda mfupi sana wa kuhakikisha maabara hizo zinakamilika na zinatumika, tuliomba shule zote 26 zipelekewe maelekezo ya kuhakikisha maabara zinakamilika na zinatumika, na tuliomba wizara ichukue hatua za dharura kuhakikisha vitendanishi vinapelekwa na vinakuwa vya kutosha,” amesema Nyamoga.
Akizungumza Naibu Waziri wa TAMISEMI, Zainab Katimba kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Mohamed Mchengerwa, amesema wamepokea maelekezo ya kamati hiyo na kusisitiza kuwa lengo la ujenzi wa shule hizo ni kuwawezesha watoto wa kike kusoma masomo ya Sayansi katika mazingira salama, yatakayowaepusha na vishawishi vinavyoweza kusababisha kukatisha masomo yao.
Sambamba na hilo ametoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini ambao wamepokea mradi wa shule hizo kuhakikisha miundombinu inakamilika kwa asilimia 100 ili wanafunzi waliokwisha ripoti shuleni wapate mazingira bora ya kusomea.
ZINAZOFANANA
Bil 3.4 zatumika kulipa fidia wamiliki wa ardhi Dodoma
NSSF kutoa mafao siku moja baada ya mwanachama kustaafu
Serikali kuwapa ulinzi wabunifu wa vifaa mbalimbali