March 14, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

OMO afunguka mazito waliyokutana nayo Angola

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman

 

MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo pia Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman ‘OMO’, ameeleze adha walizopata wakati wamezuiliwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Luanda nchini Angalo. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

OMO aliyechapisha kupitia ukurasa wake wa ‘X’ leo tarehe 14 Machi 2025 , amesema kuwa Mamlaka za Angola ziliwaachia saa nne usiku wakiwa wamechoka.

“Baada ya Mamlaka za Angola kutuzuia kwa muda wa takriban Saa Nane (8) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Quatro de Fevereiro wa Luanda, Jana Machi 13, 2025, Mimi pamoja na Viongozi wengine Mashuhuri wakiwemo Marais Wastaafu kutoka Botswana na Colombia, Waziri Mkuu Mstaafu wa Lesotho, na baadhi ya Wakuu wa Vyama vya Siasa kutoka Mataifa mbalimbali, Barani Afrika na kwengineko Ulimwenguni; hatimaye Majira ya Saa Nne (4.00) Usiku tuliachiliwa huru na kupelekwa katika Hoteli ambazo tulipangiwa, huku tukiwa na machofu.” ameandika OMO.

OMO ameandika kuwa mkasa huo haujawakuta viongozi wa upinzani pekee yao hata Balozi wa Tanzania nchini Zambia aliyekuwa kwenye msafara huo.

“Wakati hayo yakitokea, nilikuwa nimeambatana na Balozi wa Tanzania Nchini Zambia, Luteni Jenerali Matthew Edward Mkingule, ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Angola,” ameandika OMO.

OMO amekilezea kitendo hicho kuwa ni cha aibu katika mawanda ya uhusiano wa kidiplomasia”Kitendo hiki cha aibu kidiplomasia kilichotekelezwa na Mamlaka za Angola, hakikuwa na sababu hata kidogo, na kimetia doa dhana ya Umoja wa Afrika, tena katika wakati ambao Rais wa Angola ndiye Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).”

“Hiki ni Kitendo ambacho kinapaswa kulaaniwa vikali na Waafrika wote na watu wengine Duniani, wanaothamini na kutukuza misimgi ya udugu iliyowekwa na viongozi waasisi waliopigania uhuru wa Afrika,” ameandika.

OMO ameweka wazi kuwa pamoja na kuchukizwa na kitendo hicho lakini moyoni mwake hana kinyongo na wananchi wa taifa hilo kwa kuwa uhusiano wa kirafiki wa raia wa mataifa hayo haujawahi kuwa na dosari.

OMO amesema kuwa leo ameamua kurejea nchini Tanzania na kwamba hana mpango wa kuendelea kushiriki Kongamano la Jukwaa la Demokrasia lilitarajiwa lianze leo nchini Angola.

About The Author

error: Content is protected !!