March 14, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Majaliwa azindua kituo cha mabasi Nzega Mjini

 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza halmashauri ya Nzega kwa uamuzi wa ujenzi wa kituo kikubwa cha mabasi Nzega mjini ambacho ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100. Anaripoti Apaikunda Mosha, Tabora … (endelea). 

Akizungumza  leo tarehe 13 Machi 2025, katika hafla ya uzinduzi wa kituo cha mabasi Nzega, Majaliwa ameitaka halmashauri hiyo kuweka muongozo mzuri ambao utatoa fursa kwa wananchi wajasiriamali na waanzilishi wa biashara ndogo ndogo katika eneo hilo kupata nafasi za kufanya biashara zao.

Aidha, Majaliwa ametoa wito kwa halmashauri hiyo kuongeza vibanda vya wafanyabiashara badala ya vichache ambavyo vimejengwa mpaka sasa ili wananchi wawekeze kwenye biashara na kukuza mji huo.

“Kituo hiki ni kizuri na kimejengwa kwa ubora, kituo hiki kinatakiwa kianze kutumika ili wananchi waanze kunufaika nacho, Watumishi wa halmashauri ongozeni Wana-Nzega kunufaika na fursa katika eneo lenu,” amesema Majaliwa.

Amesisitiza kuwa serikali ina lengo la kutaka wananchi wengi zaidi wanufaike, hivo kupitia ubunifu huo wengi watanufaika, aidha ametoa wito kwa  halmashauri kuwashawishi na kuwawezesha wajasiriamali kuwekeza Nzega ili wapate riziki zao na kuongeza mzunguko wa fedha.

Katika hatua nyingine, Majaliwa ametoa wito kwa watumishi wa halmashauri nchini kuendelea kujielekeza katika kutatua changamoto ndogo ndogo za wananchi pamoja na kutumia mapato ya ndani kutekeleza miradi ya kimaendeleo.

“Halmashauri mnapata bilioni 3 kwa mwaka, nusu mwaka mnapata bilioni 1.5 na miezi mitatu mnapata  milioni 750 elekezeni kwenye kutatua matatizo madogo madogo ya wananchi,”amesema Majaliwa.

About The Author

error: Content is protected !!