March 13, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Asilimia 80 ya Watanzania kutumia Nishati Safi ifikapo 2034

 

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amesema serikali yetu imepanga kuwafikia asilimia 80 ya Watanzania kwa kuwawezesha kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Anaripoti Mwandishi Wetu, Bridgetown …(endelea).

Ameyasema hayo leo tarehe 13 Machi 2025, katika mkutano wa kimataifa wa matumizi ya nishati endelevu uliofanyika nchini Barbados na kuhudhuriwa na viongozi wa nchi mbalimbali.

Biteko amesema, kupitia mradi uliopo Tanzania wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unaozalisha megawati 2,115 utawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika na endelevu kwa maendeleo na ustawi wa wananchi katika ngazi mbalimbali.

Aidha, amesisitiza kuwa, utekelezaji wa lengo namba 7 katika mpango wa maendeleo ya milenia unahitaji ushirikiano miongoni mwa Serikali na sekta binafsi katika kuboresha upatikanaji wa nishati safi ikiwa ni moja ya utatuzi wa changamoto zilizopo.

Amesema ni muhimu kwa mataifa kuwekeza katika miundombinu kwa ajili ya upatikanaji wa nishati safi sambamba na kuweka mifumo ya ubunifu na utashi katika kuwezesha upatikanaji wa nishati kwa usawa bila kuacha makundi mengine.

Naye, Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Mottley amesema ni wakati sasa wa kuweka mkakati wa kimataifa na kukubaliana kushirikiana kumaliza changamoto ya upatikanaji wa nishati kwa wote.

Ametoa rai ya kufanywa kwa utafiti ili kupata ufumbuzi wa changamoto zilizopo, ufumbuzi wa ndani au kutoka katika nchi yoyote duniani kulingana na kuwa na watu zaidi ya milioni 600 barani Afrika wanaoishi bila huduma ya umeme suala ambalo limesababisha changamoto katika nchi nyingi duniani.

Vilevile Rais wa Sierra Leone,Julius Maada Bio amesema katika kipindi hiki ambapo nishati ni nyenzo muhimu katika upatikanaji wa maendeleo, ni muhimu kuwezesha watu na makundi yote kupata nishati hususani katika maeneo ya vijijini yanayokabiliwa na umasikini uliokithiri.

“Wanawake na watoto ambao wanatumia muda mwingi kutafuta nishati ambayo sio safi kwa ajili ya kupikia, wanatakiwa kuwezeshwa kupata nishati safi na hivyo kutumia muda mwingi kufanya shughuli za maendeleo,” amesisitiza Julius.

Na kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Damilola Ogumbiyi, amesema upo umuhimu wa kuweka ajenda madhubuti zitakazosaidia  kukabiliana na vitendo vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyo safi kutokana na matokeo tunayoona ya ukosefu wa nishati safi kama vile uharibifu wa mazingira unaosababisha ukame na mafuriko ambayo kwa kupata nishati safi tunaweza kuondokana nayo.

About The Author

error: Content is protected !!