March 12, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC kushirikiana na H’shauri kudhibiti upotevu wa mapato, kuunga mkono agizo la Samia

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya kushirikiana na halmashauri pamoja na mamlaka zote za tawala za mikoa na serikali za mitaa katika kuboresha ukusanyaji wa mapato kwa njia za kidijitali na kuongeza uwazi katika mifumo ya fedha ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan linalozitaka mamlaka hizo kukabiliana na upotevu wa mapato ya serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Akizungumza jana jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT), Rais Samia alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, pamoja na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanasimamia vyema ukusanyaji wa mapato ili kubaini wahusika na kuchukua hatua.

Kufuatia agizo hilo la Rais Samia, benki ya NBC ambayo ni mmoja wa wadhamini muhimu wa Mkutano wa ALAT na mdau wa huduma za kifedha kwa halmashauri hizo, kupitia kwa Mkuu wa Idara yake ya Sekta ya Umma, Joyce Maruba alielezea mkakati wa ushirikiano na halmashauri hizo kuhakikisha agizo hilo la Rais linatekelezwa kwa urahisi zaidi kupitia huduma zake kisasa kwa njia ya kidigitali hususani katika ukusanyaji wa mapato hayo ya serikali.

“Agizo hili la Rais limekuja wakati muafaka ambapo ni hivi karibuni tu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alituzindulia rasmi huduma yetu kidijitali ya ‘NBC Kiganjani’ ambayo imeboreshwa zaidi ikiwa inalenga kuwarahisishia watanzania upatikanaji wa huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo malipo mbalimbali ya serikali na hivyo kuihakikishia serikali uhakika wa kupokea makusanyo yake kwa urahisi, uwazi na bila upotevu wowote,’’ alisema Maruba wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano huo.

“Hivyo msisitizo alioutoa Rais Samia leo, kwetu ni kama chachu ya kutuhamasisha zaidi kuendelea kuwafikia watanzania wengi zaidi ili waendelee kutumia huduma hii ya kisasa na hatimaye kufanikisha maono haya ya Rais. Ombi letu kwa Halmashauri na tawala nyingine za mitaa kuendelea kushirikiana nasi kufanikisha hilo,’’ aliongeza.

Benki ya NBC imekuwa ikitoa huduma mbalimbali za kielektroniki kwa Halmashauri za Wilaya na Miji katika ukusanyaji wa mapato kupitia Mfumo wa Malipo ya Serikali Kielektroni (GePG). Uwezo huo unaimarishwa zaidi na mtandao wake mkubwa wa NBC Wakala, mashine za POS, pamoja na usimamizi wenye usalama katika malipo na ukusanyaji kwa njia rahisi zaidi za kidigitali kupitia huduma ya NBC Kiganjani.

Zaidi kupitia huduma yake ya ‘NBC Connect’ ambayo ni mahususi kwa makampuni pamoja na taasisi mbalimbali, benki hiyo imekuwa ikiwezesha upatikanaji wa huduma salama na haraka za kibenki kwa njia ya mtandao na hivyo kuchochea ufanisi na uwazi katika ufanyaji wa malipo ya taasisi na mashirika hayo.

Akizungumzia ushiriki wa benki ya NBC kwenye mkutano huo, Muruba alisema imekuwa ni kipaumbele cha benki hiyo kushirikiana na ALAT katika kifanikisha mkutano huo ikiwa kama mdhamini muhimu lengo likiwa na kupata wasaa wa kuwa karibu na viongozi wa halmashauri mbalimbali hapa nchini ambazo zimekuwa zikihudumiwa na benki hiyo kupitia huduma zake mbalimbali ikiwemo huduma za malipo na mikopo kwa halmashauri husika pamoja na wafanyakazi.

“Kwetu kama benki ni heshima kubwa kuwa mshirika muhimu katika ajenda ya maendeleo ya kitaifa, na tunahakikisha tutaendelea kuwa sehemu ya mkutano huu kama ambavyo milango yetu imeendelea kuwa wazi ili kutumikia si tu serikali na watumishi wa umma lakini Watanzania wote kwa ujumla.”

“Zaidi tunaendelea kuhusika katika miradi muhimu ya serikali ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi ikiwemo miradi wa ujenzi kupitia uwezeshaji wa namna tofauti ikiwemo usimamizi na uuzaji wa Hati fungani. Pia tumekuwa tukisaidia vikundi maalum kama wajasiriamali, mnyororo wa thamani ya kilimo, AMCOS, Wamachinga, vijana waendesha pikipiki ‘bodaboda’, na makundi mengine,” alihitimisha Maruba.

About The Author

error: Content is protected !!