March 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Sarungi alijitolea kuwa mlezi wangu bungeni – Zitto Kabwe

 

WAZIRI wa zamani wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Philemon Sarungi amefariki tarehe 5 Machi 2025 saa kumi jioni jijini Dar es salaam, taarifa ya kifo chake imetolewa na msemaji wa familia hiyo Martin Leonard Sarungi. Anaripoti Apaikunda Mosha, Dar es Salaam … (endelea).

Baada ya kutangazwa taarifa hiyo mwanachama na Kiongozi wa zamani wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe kupitia kurasa wake wa X ameandika historia yenye simulizi fupi kuhusu maisha yake na Hayati Sarungi.

Zitto ameandika hivi “Nilipochaguliwa kuwa Mbunge mara ya kwanza mwaka 2005 nilipata Wazee 3 kama walezi wangu Bungeni kwa kujitolea wao. Mzee William Shelukindo alinifundisha namna nzuri ya kuandika maswali ya Bungeni.”

“Mzee Jackson Makweta na Prof Philemon Sarungi walikuwa wakinichukua kwenda kunywa chai/kahawa mara kwa mara kuchambua nilichozungumza bungeni na kunionyesha maeneo napaswa kuboresha.”

“Miaka 5 ya mwanzo Bungeni nilijengwa na kupewa ujasiri pamoja na watu wengine, wazee hawa. Kupitia malezi hayo ya Mzee Sarungi ndipo nilikutana na binti yake @MariaSTsehai kwa mara ya kwanza katika viunga vya Bunge mwaka 2006.”

“Mzee Sarungi aliendelea kuwa Mzee wangu kwa muda mrefu akinipa nasaha katika vipindi mbalimbali vya maisha yangu ya Siasa. Ni Mzee mwenye historia kubwa ya namna ya kusoma kwake, kuwa daktari, diwani, mkuu wa mkoa, Waziri na Mbunge wa kawaida.”

“Akiwa Waziri wa Ulinzi Jenerali Mboma alikuwa amemaliza muda wake na uteuzi wa CDF mpya ulipaswa kufanyika. Hii ni moja ya simulizi nilikuwa napenda arudie mara kwa mara kwangu iliyonifunza nafasi ya Mawaziri wa Ulinzi katika mchakato wa kumpata Mkuu wa Majeshi.”

“Hatimaye Jenerali Waitara aliteuliwa na Prof Sarungi ndiye aliyemfuata nyumbani kwake kumpeleka ikulu kwa Rais Mkapa kuelezwa uteuzi huo. Mzee Sarungi alikuwa kila akinisimulia hili anacheka sana. Ni simulizi nzuri ya ‘siasa za uteuzi’ kwenye majeshi.”

Zitto amemaliza kwa kuandika hivi “Mzee Sarungi ametangulia mbele ya haki. Mzee mwema sana. Mzalendo. Mlezi. Salaam zangu za rambirambi kwa ukoo wa Sarungi, watoto wote, ndugu jamaa na marafiki. Hamba Kahle Tata”

About The Author

error: Content is protected !!