March 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mwanafunzi wa chekechea afariki kwa kugongwa na basi, wananchi wafunga barabara

 

WANANCHI wa kata ya Igunga wilaya ya Igunga, Tabora wamefunga barabara kuu itokayo Mwanza kwenda Dar es Salaam baada ya basi la kampuni ya Nyehunge lenye namba za usajili T610 EFG kumgonga mwanafunzi mdogo aliyefahamika kwa jina la Queen Jackson (5) mwanafunzi wa darasa la awali shule ya msingi Jitegemee. Anaripoti Abdallah Amiri, Igunga … (endelea).

Wakizungumza kwa uchungu wananchi hao wameliomba Jeshi la Polisi wilaya ya Igunga na TANROAD mkoa wa Tabora kuhakikisha wanazuia ajali katika eneo hilo la Hanihani kwani limekuwa likigharimu maisha ya wanafunzi na kusababisha hata ulemavu kwa baadhi ya wananchi.

“Kiukweli tumechoka na vifo vya watoto wetu, nimeishuhudia hii ajali mtoto alikuwa akitoka shule huku basi la Nyehunge likiwa na mwendokasi wakati dereva akimuona kabisa mtoto huyo. Laiti angekuwa mwendo wa kawaida asinge mgonga huyu mtoto, inatia huruma sana,”  alisema Deo Zakaria.

Huku Elisante Peter mkazi wa Hanihani, alisema kuwa mabasi mengi yamekuwa yakipita katikati ya mji wa Igunga kwa mwendokasi, hivyo wameliomba Jeshi la Polisi kuwa na askari katika maeneo yote ya kati ya mji ili kudhibiti mabasi na malori yanayopita kwa mwendokasi.

“Mimi niliwahi kugongewa mtoto wangu wa darasa la pili katika hii hii barabara na viongozi walituahidi kutujengea shule upande wetu huu wa Hanihani na waliahidi kutuwekea bamsi na traffic kuwa katika hili eneo, sasa tunaomba tujengewe shule upande wetu kwani wenye watoto tunateseka kweli,” alisema Tabitha Ally kwa uchungu.

Naye, Yona Masasi alisema kuwa mpaka sasa ni watoto watano wameshafariki dunia kwa kugongwa na mabasi na malori yanayopita kwa mwendo kasi wa zaidi ya spidi 80 pasipo kuzingatia sheria na miongozo ya usalama barabarani.

Mkuu wa Oparesheni wa Jeshi la Polisi Igunga, aliyejitambulisha kwa jina moja la Afande Temba, aliwaomba wananchi hao kuondoa vizuizi hivyo kwani barabara hiyo inatumiwa na wananchi wengi ikiwa ni pamoja na kutoka nje ya nchi na mikoa mingine hivyo aliyesababisha tukio hilo ni dereva wa basi la Nyehunge, kwa hiyo waachiwe wananchi wengine waendelee na shughuli zao za kiuchumi.

Akithibitisha kuupokea mwili huo wa Queen Dk. Godfrey Madebele alisema  wameufanyia uchunguzi mwili huo na kuukabidhi kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

“Ni kweli tumepokea mwili wa mtoto Queen mwenye umri wa miaka mitano ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Jitegemee ambaye inasemekana amegongwa na gari, mpaka sasa mwili tumeisha ufanyia uchunguzi na tumeisha ukabidhi kwa ndugu,” alisema Dk. Madebele.

Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishina Msaidizi Constatine Mbogambi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, iliyotokea tarehe 4 Machi 2025, majira ya saa 05:05 asubuhi, katika barabara kuu itokayo Mwanza kuelekea Dar es salaam.

Alisema ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa dereva, Rashid Mussa Bakari (32) wa basi la kampuni ya Nyehunge lenye namba za usajili T610 EFG lilikuwa likitokea Mwanza kuelekea Moshi.

Kamanda Mbogambi alibainisha kuwa baada ya kugongwa mwanafunzi huyo wananchi walifunga barabara hadi alipofika kaimu mkuu wa polisi Igunga na kuzungumza na wananchi hao, na ndipo walitoa vizuizi vyote vilivyokuwa barabarani. Dereva wa basi anashikiriwa na jeshi la polisi Igunga.

Mazishi ya mwanafunzi huyo yamefanyika leo tarehe 5 Machi 2025 katika makaburi ya Nkokoto, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo alihudhuria mazishi hayo.

About The Author

error: Content is protected !!