
Mwenyekiti wa BAVICHA, Wakili Deogratius Mahinyila
MWENYEKITI wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA), Wakili Deogratius Mahinyila, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda kutoa ufafanuzi juu ya kauli yake ya dhati na itahakikisha Katibu wa vijana wa chama hicho Amani Manengelo anapatikana. Anaripoti Apaikunda Mosha Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na vyombo vya habari leo tarehe 3 Machi 2025, Wakili Mahinyila amesema, tangu kupotea kwa Amani mpaka sasa ni siku 18 zimepita bila mafanikio yoyote ya kupatikana kwake, amesema huwenda kauli hiyo ilikuwa kwa ajili ya kuwaridhisha tu na sio ya dhati.
“Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alishatoa ahadi kuwa Amani Manengelo atapatikana mpaka leo siku ya 18 hajapatikana hiyo kauli ya kwamba, Amani anapatikana na siku zinakwenda, Amani hapatikani, unatuambia nini kuhusu hii kauli yao sio ya kutupumbaza tu,” amesema Mahinyila.
Pamoja na hayo Mahinyila amesema kuwa ni vema viongozi wa umma watambue kuwa sio kila maneno ni sahihi kutamka, hii ni kutokana na kauli aliyotumia Mtanda wakati anawaalika vijana waliopanga kwenda ofisini kwake kwa lengo la kupata muafaka wa alipo Amani aliyepotea.
“.. anasema mnaomtafuta Amani viongozi wa CHADEMA, njoeni ofisini nitawaandalia na chai watu wamempoteza ndugu yao hawajui alipo. Hivi Mtanda angekuwa amepotea mwanao halafu kuna kiongozi wa umma anakuambia njoeni tuzungumze mtakuta nimewaandalia na chai mtu aliyepoteza ndugu hiyo nguvu ya kunywa chai anaipata? utuambie Mtanda Manengelo ulisema atapatikana atapatikana lini? Kwa vile umetuhakikishia atapatikana pengine unajua alipo,” amesisitiza hilo Mahinyila.
Aidha Mahinyila amesema kuwa asilimia kubwa ya vijana ambao wanatekwa ni vijana wa upinzani na vijana wanaharakati, na kwa kuwa watu wanaotekwa ni watu wenye mrengo wa kimageuzi ni watu wanaoiunga CHADEMA mkono, basi jambo hili linafanya waamini kutekwa kwao ni kwa lengo la kupunguza ari na morali ya vijana wa upinzani kuendelea kuikosoa serikali.
“…. kwanini tusiamini huu ni mkakati wa kupunguza kasi yetu ya kuwa wapinzani. Ni kikundi gani kina maslahi na vijana wa CHADEMA. Polisi mtuambie hawa watu ambao wanaotuteka vijana wa chadema, wanaowateka vijana ambao wana maoni tofauti na serikali,” amesema Mahinyila.
ZINAZOFANANA
Puuzeni propaganda za upinzani uchaguzi utafanyika – Makalla
TONE TONE ya Chadema yafika Mil 64
Wananchi wa Mahomanyika wampigia magoti Rais Samia mgogoro wa ardhi