February 27, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

ACT waitaka Serikali kufuta mkataba na mwekezaji Bandari ya Z’bar

Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa

 

CHAMA cha ACT Wazalendo kimeitaka serikali ya Zanzibar kuvunja mkataba na mwekezaji wa Bandari hiyo kwa sababu ameshindwa kutekeleza yale yaliyoahidiwa hivyo anatakiwa kurudisha bandari hiyo kwa Shirika la Bandari la Zanzibar. Anaripoti Apaikunda Mosha. Zanzibar … (endelea).

Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Ismail Jussa amewaeleza waandishi wa habari, Alhamisi 27 Februari 2025 kuwa uwekezaji uliofanyika katika Bandari ya Zanzibar ni udanganyifu, serikali inawezaje kutumia fedha za walipa kodi kiasi cha Sh. 17 bilioni kununua vifaa vya Bandari na kuweka mfumo wa E- Port wakati kuna mwekezaji.

“Vituko vilikuwa vikifanyika wakati wa kuweka saini katika hicho kilichoitwa uwekezaji wa kimataifa, kwani utiaji wa saini ulifanyika kienyeji tena wakati wa usiku na mwekezaji alikuwa African Global Logistics(AGL) badala ya BALOR ya uingereza iliyotangazwa mwanzo, mbali na hiyo hata hiyo AGL hatukuiona baadae tukaletewa Zanzibar Multipurpose Terminal (ZMT),” amesema Jussa.

Amesema zipo sheria zimewekwa ambazo ni Sheria ya manunuzi ya umma, kwenye eneo la taratibu za zabuni, pale serikali inapotaka kununua bidhaa au kupata/kutoa huduma ya jambo fulani, pamoja na sheria ya ushindaji wa haki (fear competition).

“Ubabaishaji mapema ulionekana, hakukutangazwa zabuni na wala hakukufanyika uchunguzi wa kujiridhisha kwamba ni nani hasa huyo mwekezaji, ambae anataka kukabidhiwa lango kuu la kuingilia na kutoka Zanzibar kwa maana ya Bandari kuu ya nchi,” ameeleza Jussa.

Ameeleza kuwa Serikali ya Zanzibar iliahidi uwekezaji huo ulioitwa wa kimataifa katika Bandari ya Zanzibar kuleta mabadiliko na mafanikio makubwa kwa wananchi, walitoa ahadi nyingi zote zilikuwa ni kuwalaghai wananchi wake, kati ya mengi aliyosema Rais Mwinyi wakati huo hakuna hata moja limefanyika zaidi amezidi kuwakandamiza masikini.

“Na hata, Waziri wa Ujenzi mawasiliano na uchukuzi Khalid Salum alipoulizwa kuhusu Kampuni na kama serikali imeifanyia tathmini iliyopewa Bandari hiyo alijibu kuwa kampuni ni nzuri na inafahamika kimataifa, kwa hiyo serikali haikuona haja ya kuifanyia uchinguzi kwa sababu tayari imejiridhisha kuhusu uwezo wake,” amesisitiza Jussa.

Amesema dhumuni la kusema hayo ni kwasababu wakati wa majadiliano ya uwekezaji huo hata timu ya majadiliano ya serikali (government negotiation team) ilikuwa inasukumwa mpaka watu muhimu kutoka serikalini kutoka timu hiyo walijitoa kwa sababu ya kutokubaliana na kilichokuwa kinafanyika.

Amesema hali ya sasa inawaumiza watumiaji wa Bandari ya Zanzibar na wananchi huku mwekezaji anajipatia faida kubwa, hakuna hata jambo moja lililoahidiwa limetimia isipokuwa changamoto zimezidi kushamiri hasa kuelekea kipindi hichi cha Ramadhani.

About The Author

error: Content is protected !!