February 21, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

SBL yazindua kampeni ya SMASHED kukabiliana na unywaji wa pombe chini ya umri

KAMPUNI ya Serengeti Breweries Limited (SBL) imezindua kampeni yake ya kukabiliana na unywaji wa pombe kwa vijana chini ya umri inayojulikana kama SMASHED jijini Mwanza, ikionyesha dhamira yake ya kukomesha unywaji wa pombe kwa vijana kupitia elimu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Mkolani iliwakutanisha maafisa wa serikali, viongozi wa elimu, na wadau wa sekta ya biashara.

Akiongoza uzinduzi huo, Christopher Ngubiagai, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe kwa niaba ya Said Mtanda, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alisifu mpango huo kwa kusema: “Unywaji wa pombe kwa vijana chini ya umri unaathiri siyo tu mtu binafsi bali pia jamii kwa ujumla. Programu ya SMASHED ni hatua muhimu katika kuwaelimisha na kuwawezesha vijana wetu kufanya maamuzi sahihi. Nawapongeza SBL kwa jitihada hizi muhimu zinazolingana na malengo yetu ya kuwalinda na kuwaendeleza vijana wa Kitanzania.”

“Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021, SMASHED imefikia zaidi ya wanafunzi 30,000 katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, na Kilimanjaro. Leo, tunajivunia kuupanua mpango huu hadi Mwanza, kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata maarifa muhimu yanayowasaidia kufanya maamuzi bora kwa maisha yao,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi.

Anyalebechi aliongeza kuwa lengo la SBL ni kuendelea kusambaza mpango huo kote nchini, kufikia shule na jamii nyingi zaidi ili kuleta mabadiliko ya kudumu.

SMASHED ilianza kama mpango wa kimataifa unaolenga kukabiliana na unywaji wa pombe kwa vijana waliovuka umri kupitia elimu ya kielektroniki na maonyesho ya michezo. Mpango huu unatekelezwa kwa ushirikiano na shule, serikali za mitaa, na mashirika yanayolenga vijana. Unawapa wanafunzi ujuzi wa maisha halisi na uelewa wa athari za matumizi mabaya ya pombe.

Kupitia Spirit of Progress, SBL inabaki na dhamira ya kuimarisha jamii endelevu kwa kuwawezesha vijana kufanya maamuzi sahihi kuhusu unywaji wa pombe na kujenga mustakabali mzuri wa Tanzania.

About The Author

error: Content is protected !!