February 21, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

DAWASA wajitia kitanzi changamoto za maji Temeke

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama

 

KAIMU Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) Mhandisi Mkama Bwire amesema DAWASA inatambua na itashughulikia changamoto ya huduma ya maji wilaya ya Temeke ambapo bado wanatumia mitambo ya zamani pamoja na visima. Anaripoti Apaikunda Mosha. Dar es Salaam … (endelea). 

Akizungumza katika ufunguzi wa Kikao Kazi na Wenyeviti wa Serikali za mitaa leo tarehe 20 Februari 2025, katika Wilaya ya Temeke, Mhandisi Bwire amesema DAWASA bado inaona umuhimu wa viongozi wa mitaa katika usimamizi wa karibu wa huduma za Majisafi na usafi wa Mazingira.

Amesema pia kwa kushirikiana na hao viongozi wa mtaa wenye dhamana ya wananchi, changamoto hizo za maji kwa wananchi zinaweza kutatulika kwa kiwango kikubwa sana kwa kuwa DAWASA wanatambua kuwa hali ya huduma ya maji katika wilaya ya Temeke sio nzuri, jumla ya kata 23  pamoja na mitaa142 mtandao mkubwa wa maji haujawafikia.

“Lazima tuwe na mambo ambayo tunataka kushirikiana na kujenga uelewa wa pamoja wakati tunapokwenda kuhudumia wananchi kile atakachosema Mwenyekiti basi kiwe hicho hicho atakachosema DAWASA,” amesema Bwire.

Pamoja hayo Bwire amesema atawaonyesha hali halisi ilivyo katika maeneo hayo na pia kupokea maoni  ya wenyeviti ili kujenga uelewa na mikakati ya pamoja itakayosaidia kuwezesha uboreshwaji wa huduma ya maji.

Aidha, Bwire amesema kuwa anataka kuirudisha DAWASA iwe ni ya wananchi, hivyo watawezesha wenyeviti wa mitaa kutatua baadhi ya changamoto ndogo ndogo zinazoweza kutatulika, kama vile maji kumwagika, wizi wa miundombinu na changamoto za usomaji wa bili ili kurahisisha utendaji wa kazi.

 

About The Author

error: Content is protected !!