
KAMPUNI ya Maendeleo Hospitality Ventures (MHV), inayoongozwa na wawekezaji wa Kimarekani, imetangaza mpango wake unaolenga kujenga hoteli ya kifahari yenye hadhi ya nyota tano katika Kijiji cha Robanda, karibu na Lango la Fort Ikoma la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mpango huu unalenga kuimarisha sifa ya Tanzania kama eneo lenye hadhi ya juu la kutembelea, kuhamasisha ukuaji wa uchumi wa eneo husika sambamba na kuongeza fursa za ajira kwa jamii inayozunguka eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mwekezaji huyo mapema leo, hoteli hiyo inatarajiwa kuwa mfano wa huduma za kimataifa, ikitoa fursa kwa wageni kupata wasaa wa kuwatazama wanyapori kwa mvuto zaidi ili kufurahia kwa ukamilifu uzuri wa asili ambao hifadhi ya Serengeti inajipambanua nao.
Zaidi mwekezaji huyo amethibitisha nia yake ya kuchochea utalii endelevu kupitia uoneshaji wa urithi wa utamaduni wa Tanzania huku akihakikisha kuwa jamii za eneo hilo zinanufaika na mafanikio ya kiuchumi kupitia hoteli hiyo.
Kupitia taarifa hiyo, Mwenyekiti wa MHV, Rishen Patel, alieleza furaha yake kuhusu mradi huo muhimu, akisema, “Maono yetu ni kubadilisha huduma za hoteli nchini Tanzania kupitia hoteli za kifahari zinazosherehekea urithi wa kiutamaduni na mandhari nzuri. Serengeti, inayojulikana kwa wanyamapori wake wa kipekee na Uhamaji Mkubwa wa Wanyama, ni mahala sahihi kwa ajili ya mwanzo wa safari yetu.”
Patel alitilia mkazo maendeleo makubwa ya sekta ya utalii ya Tanzania katika muongo uliopita, ambapo imeshuhudiwa idadi ya watalii ikifikia kiwango cha kihistoria cha watalii milioni 1.8 mwaka 2023, ikileta mapato ya Dola za Kimarekani 3.37 bilioni.
Takwimu za awali za Agosti 2024 zinaonyesha ongezeko kubwa la wageni wa kimataifa hadi kufikia zaidi ya watalii milioni 2 huku mchango wa kiuchumi ukitarajiwa kufikia Dola za Kimarekani 3.5 bilioni. “Mwelekeo huu hauoneshi tu maslahi ya kimataifa kwa Tanzania kama eneo maarufu la utalii lakini pia unasisitiza juhudi za serikali zinazokusudia kuboresha miundombinu na kuendeleza mikakati ya utalii endelevu.’’ Alibainisha.
Aidha Patel alidokeza kuhusu nia ya wazi ya mwekezaji huyo kutafuta ushirika wa ndani katika kufanikisha mpango huo. Katika kufanikisha nia hiyo alisema kampuni ya MHV ipo kwenye ushirikiano na kampuni ya CORE Securities Limited ambayo ni mwanachama wa soko la hisa la Dar es Salaam mwenye leseni ili kupata mtaji kupitia ofa ya umma.
“Mpango ulivyo ni kuorodhesha asilimia 31 ya hisa mahsusi kwa wawekezaji wa Kitanzania, huku asilimia 3 ikitengwa kwa jamii za eneo husika la mradi na asilimia 2 nyingine kwa wafanyakazi wa mradi huo lengo likiwa ni kuimarisha ushirikishwaji na uwezeshaji wa jamii.’’
“Tunaamini huu ni wakati sahihi kwa utambulisho wa uanzishwaji wa mradi huu wenye ushirikishwaji wa umma’’ alisema Patel huku akiongeza: “Tuko tayari kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya malazi ya kiwango cha juu yanayoakisi viwango vya kimataifa. Hoteli yetu ya kisasa katika hifadhi ya Serengeti ni mwanzo tu kwa kuwa tunatarajia miradi mingine katika maeneo ya Zanzibar, Ngorongoro, na Kilimanjaro tukilenga kuvutia wageni kutoka kote ulimwenguni.”
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya CORE Securities Limited, CPA George Fumbuka, alithibitisha jukumu muhimu la kampuni hiyo katika kuratibu Ofa ya Umma ya Kwanza (IPO) ya MHV. Alibainisha kuwa kampuni hiyo iko katika mazungumzo ya kina ili kuanzisha Timu ya Ushauri itakayowezesha kupata vibali muhimu vya kiserikali kuelekea izunduzi wa Ofa hiyo kwa Umma ndani ya mwezi ujao.
“Ratiba hii yenye matumaini inaendana na lengo la MHV la kuzindua hoteli yake ya kifahari ifikapo Julai 2025.’’ Alisema Fumbuka huku akionyesha matumaini kuhusu mpango huo
“Tunajivunia kuwa sehemu ya mradi huu wa kipekee, ulio na msaada wa sifa za kimataifa za Mwekezaji na ujuzi wa kibiashara. Tunawapongeza MHV kwa kufanya uamuzi sahihi, kwani watawasaidia Watanzania wengi kupitia umiliki mpana wa hisa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam,” aliongeza.
ZINAZOFANANA
Exim yazindua suluhisho la malipo ya kisasa katika Z-Summit 2025
CANDY’S Bonanza kukupa mtonyo leo
Mamilioni yanatoka kirahisi ukicheza Teen Patti Poker