
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ametoa agizo la marufuku kwa wageni kuingia na kufanya shughuli za uchimbaji kwenye leseni za wachimbaji wadogo. Hatua hii inakuja baada ya kubainika kwa changamoto nyingi zinazohusiana na mikataba ya utoaji msaada wa kiufundi kati ya wachimbaji wadogo na raia wa kigeni. Anaripoti Yusuph Kayanda, Morogoro … (endelea).
Akizungumza katika kikao kazi kilichofanyika leo Februari 17, 2025, katika ukumbi wa Edema Hoteli, mkoani Morogoro, Waziri Mavunde alisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria na kutoa wito kwa washiriki wa kikao hicho kutoa maoni yao kwa uwazi ili kusaidia kuandaa kanuni bora za kusaidia wachimbaji wadogo.
“Katika kipindi cha hivi karibuni, tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika sekta ya madini, na tunataka kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wanapata msaada wa kutosha ili waweze kujiendeleza. Hatuwezi kuruhusu wageni kuingia na kuharibu mfumo huu,” alisema Waziri Mavunde.
Waziri aliongeza kuwa, “Haiwezekani mgeni kuingia kwenye leseni ya mchimbaji mdogo bila kufuata utaratibu. Hii inawanyima wachimbaji wadogo fursa ya kuendelea na teknolojia na mitaji. Tunahitaji kuhakikisha kuwa sheria inatekelezwa ili kuwalinda wachimbaji wetu.”
Aidha, Waziri Mavunde alitoa onyo kali kwa wachimbaji wanaoingiza wageni bila kufuata taratibu, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa ikiwa sheria zitakiukwa. Alitoa wito kwa Maafisa Madini nchini kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kudhibiti uingiaji wa wageni kwenye leseni za uchimbaji mdogo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, alieleza kuwa kikao hicho kinatoa fursa kwa wadau kutoa maoni yao ili kusaidia kuandaa rasimu ya kanuni zinazohusiana na msaada wa kiufundi kwa wachimbaji wadogo.
Rais wa Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini, John Bina, alipongeza hatua ya Waziri Mavunde ya kuwashirikisha wadau katika mchakato wa kuandaa kanuni, akisema kuwa ni muhimu kwa, maendeleo ya sekta hiyo.
ZINAZOFANANA
SBL yazindua kampeni ya SMASHED kukabiliana na unywaji wa pombe chini ya umri
DAWASA wajitia kitanzi changamoto za maji Temeke
Uingereza yafurahishwa na maboresho Bandari ya Dar, yaipongeza serikali