February 11, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Jafo ataka watanzania wachamkie fursa za AGOA, azindua Bodi ya Uongozi wa CBE

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Seleman Jafo

 

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk Seleman Jafo, amekitaka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kujitangaza nje ya mipaka ya Tanzania ili kiweze kupata wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea). 

Amesema badala ya kutegemea wanafunzi wa ndani pekee chuo hicho kina uwezo wa kupata wanafunzo kutoka mataifa mbalimbali kwani taaluma inayotolewa chuoni hapo inakidhi vigezo vya kimataifa.

Aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua rasmi Bodi ya Uongozi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) .

Pia aliwataka vijana wasomi nchini kushirikiana na kampuni mbalimbali za uzalishaji kutumia fursa ya ukuaji wa Fursa za Afrika (AGOA) kupeleka bidhaa nyingi kutoka Tanzania kwenye soko la Marekani.

Amesema fursa ya soko hilo inatoa fursa ya aina 6,500 za bidhaa kuingia Marekani lakini bado halijatumika ipasavyo kuchangia ukuaji wa kipato cha watanzania na taifa kwa ujumla hivyo kuna umuhimu wa kuchangamka kuzipita nchi zingine.

Alisema chuo cha CBE kinawajibu wa kuandaaa vijana mahiri wanaoweza kushiriki kwenye biashara za kitaifa na kimataifa wakiwa na ujuzi uliokamilika hivyo kumudu kushindana na wenzao kimataifa.

“Nchi yetu imefunguka kimasoko tunahitaji vijana mahiri wenye ufahamu wa kutosha wa kutumia fursa za masoko zilizopo kufanya biashara za kimataifa. Vijana wakiwa na maarifa wakishirikiana na wazalishaji watauza sana bidhaa nje ya nchi,” alisema

“Kwenye AGOA tumefanya vizuri lakini tunatakiwa kufanya vizuri zaidi ya hapo na kwenye nchi za Afrika kuna soko kubwa lakini tunawajibu wa kuwawezesha vijana kuyafikia masoko makubwa kama ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC,” alisema

Alisema CBE ina dhamana ya kuwapa maarifa wafanyabiashara nchini kuhusu namna bora ya kushiriki kwenye biashara ya kimataifa kwa kuwapa mafunzo ya mara kwa mara ya muda mfupi.

“Ni imani yangu kuwa bodi hii mpya itakuwa na jicho la kuangalia fursa mbalimbali za biashara za kufanya nchi iweze kusonga mbele, jitahidini kutengeneza watanzania mahiri wenye uwezo wa kutumia fursa hizi za masoko,” alisema Waziri Jafo

Aidha, aliipongeza CBE kwa kufanikiwa kuwapa mafunzo ya biashara wafanyabiashara wadogo wadogo zaidi ya 2,000 namna bora ya kufanyabiashara na alikitaka kuandaa mafunzo kwa wafanyabiashara wengine ili kuwaongezea maarifa ya biashara.

“Andaaeni program za muda mfupi kuhusu masuala ya uongozi, namna ya kufanya usahili wa kazi, kuandika barua ya kuomba kazi kwa wiki moja au mbili mkawapa watu maarifa ya kuwa mahiri kwenye sekta ya biashara, najua mnatoa mafunzo mengi lakini ongezeni kwasababu watu wanataka maarifa ya biashara,” alisema

Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga aliipongeza bodi iliyopita kutokana na mafanikio makubwa iliyopata katika kipindi cha uongozi wake kuanzia 2021-2024 ikiwemo kutengeneza dira ya miaka 50 ya chuo hicho inayoanzia 2025 mpaka 2075.

Alisema bodi iliyomaliza muda wake imefanikiwa kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi kwani ilipoanza mwaka 2021 kulikuwa na wanafunzi 10,034 lakini mpaka inamaliza muda wake ilifanikiwa kuongeza wanafunzi hadi 22,263 karibu nusu ya wanafunzi waliowakuta.

Alisema bodi hiyo imekiwezesha chuo kupanua program zake kutoka astashahada hadi Shahada za Uzamili na kufikia program 63 na pia kutoa Shahada za Umahili (online masters program) na zimesaidia wanafunzi kusoma bila kuhudhuria darasani.

Alisema bodi pia imefanikiwa kuanzishwa kwa program ya Shahada ya Uzamivu katika biashara ya infomatiki ambapo wadau mbalimbali wameshirkishwa kutoa maoni yao kwaajili ya kuiboresha na kupata ithibati ya kuanza kutumika.

Alisema walifanikisha pia kuboresha miundombinu ya chuo hicho ambapo mwaka 2023 walianza ujenzi jengo la metrolojia wa orofa 10 utakaogharimu bilioni 22.4 ambapo awamu ya kwanza inatarajiwa kukamilika Juni mwakani.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Hashil Abdalah, alisema chuo hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa kufanya tafiti mbalimbali za maboresho ya biashara.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Zacharia Mganilwa, alisema anafahaamu kuwa ili uchumi wa nchi uweze kukua kwa kasi wanahitajika wataalamu wenye ujuzi na maarifa hivyo utakuwa wajibu wa chuo kuhakikisha wataalamu hao wanapatikana.

About The Author

error: Content is protected !!