February 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Chuo Finland na CBE watengeneza mtaala wa PhD ya infomatiki za biashara

 

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kinatarajia kuanzisha program ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Infomatiki ya Biashara ili kuleta mabadiliko ya uchumi wa kidijitali na teknolojia katika kufanya biashara za kidijitali kuendana na mabadiliko ya dunia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya kujadili mtaala wa masomo hayo yaliyowashirkisha wataalamu wabobezi kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu.

Wataalamu hao walikuwa wakipitia mtaala ambao umeandaliwa na chuo hicho na kutoa maoni yao ili baada ya hapo upelekwe kwa mdhibiti ambaye ni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTIVET) kwaajili ya kupewa ithibati na kuanza kutumika.

Alisema kuanzishwa kwa shahada hiyo ni hatua muhimu yenye kuleta mabadiliko katika kuendeleza elimu ya juu, kukuza uvumbuzi wa kiteknolojia na kuchangia ajenda ya maendeleo ya taifa.

Alisema CBE ambayo inakampasi nne nchini kwa muda mrefu imekuwa kinara katika kutoa program mbalimbali za kitaaluma na kwa kushirikana na Chuo Kikuu cha Ufini ya Mashariki kimeandaa mtaala wa informatiki za biashara.

Alisema Shahada ya PhD kwenye infomatiki za baishara ni muhimu kwani inachanganya utaalamu wa biashara na uvumbuzi wa kiteknolojia ikilenga uchanganuzi wa data, mifumo ya habari, mabadiliko ya dijiti na utafiti unaotegemea suluhisho.

“Wahitimu wa program hii wanatafutwa sana kwenye sekta ya umma na binafsi na watakuwa wahusika wakuu katika kuleta mabadiliko ya teknolojia katika tasnia mbalimbali nchini,” alisema

Alisema mtaala huo utawapa wanafunzi wa Tanzania ujuzi unaohitajika ili kuendesha na kuongoza katika uchumi wa kidijitali na kuchangia katika uboreshaji wa maendeleo ya viwanda.

Alisema mtaala huo utasaidia kuongeza tija katika biashara za kidijitali na kuimarisha ushindani wa kimataifa pamoja na kuongeza ujuzi katika kufanya tafiti na uvumbuzi wa kiteknolojia katika sekta ya biashara za kidijitali.

“Mkutano huu ni muhimu katika kuunda mustakabali wa program hii na maoni yenu wadau yatasaidia kuunda mtaala unaoakisi mahitaji ya soko la ajira na kuendana na malengo ya maendeleo Tanzania,” alisema

Alisema wanatarajia baada ya kupata ithibati mtaala huo utaanza kutumika hapa nchini na utakuwa mtaala wa kwanza kwenye biashara ya infomatiki ambao utaenda kuzalisha wataalamu watakaokuwa watafiti wabobezi katika uvumbuzi wa kiteknolojia na kuangalia mifumo itakayosaidia kwenye biashara.

“Hivi sasa teknolojia inabadilika kwa haraka sana na kuna akili mnemba (AI) yote tumeyazingatia kwenye huo mtaala na juhudi kama hizi tulianza mwaka 2014 ambapo tuliingia makubaliano na chuo cha Finland Mashariki ambao wanatoa program hiimuda mrefu,” alisema na kuongeza

“Walitusaidia sana kuwapa mafunzo wataalamu wetu ambao tumekuwa tukiwapeleka kwenye chuo hicho na mpaka sasa tuna walimu wengi ambao wameshahitimu kwenye shahada ya infomatiki ya biashara Finland na sita bado wanaendelea na masomo yao huko huko,” alisema

Angela Runyoro ambaye Mhadhiri Mwandalizi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), alisema mitaalahiyo itawezesha kuwafundisha watu kutoka ndani nan je ya nchi kupata ujuzi wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA katika biashara.

“Kwa sasa TEHAMA inahitajika katika sekta zote, hakuna namna unaweza kufanya jambo ukaikwepa na CBE wenyewe wamejikita kuanza kutengeneza wataalamu wa infomatiki za biashara kwa kujua mifumo ya kuendesha biashara kisasa,”alisema

“Hawa wataalamu watafundisha wengine watafanya tafiti watachambua mifumo inayofaa katika teknolojia ya kustawisha biashara ili watu wasifanye baishara kizamani . Hii itakuwa na manufaa sana kwa wafanyabaishara na nchi na ulimwengu kwa ujumla,” alisema Dk. Angela.

About The Author

error: Content is protected !!