January 30, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali yaridhishwa na ujenzi wa barabara Mtili-Ifwagi, Wenda-Mgama

 

MTENDAJI Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, amesema serikali inaridhishwa na kazi zinayofanywa na wakandarasi wanaojenga barabara za Mtili – Ifwagi (Km. 14) na Wenda – Mgama (Km. 19) ambazo zinagharimu Sh. 52 bilioni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Iringa … (endelea).

Barabara hizo zilizopo mkoa wa Iringa, zinajengwa chini ya mradi wa RISE, unaofadhiliwa kupitia mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia, ukiwa na lengo la kurahisisha usafirishaji wa mazao ya misitu, mboga mboga, chai, na mazao mengine kutoka mashambani hadi sokoni kwa wakati.

Akizungumza baada ya kuongoza kamati zinazohusika na usimamizi wa mradi huo katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi, Mhandisi Seff amesema miradi hiyo ipo katika hatua nzuri na akawataka wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha kazi kwa wakati uliopangwa ili kuboresha huduma kwa wananchi.

Aidha, amewataka wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya miradi kuwa walinzi wa kwanza wa barabara hizo ili kuzuia hujuma na wizi unaofanywa na watu wasio waaminifu, jambo ambalo limekuwa likisababisha hasara kwa serikali na kuhatarisha usalama wa miradi hiyo.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Seff ameagiza mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara ya Ilula Image – Ilambo (Km. 40) kurejea kazini mara moja ili kukamilisha kazi hiyo na kuondoa vikwazo vya mawasiliano vilivyopo kwenye barabara hiyo.

Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hii ili kuhakikisha wananchi wananufaika kwa wakati na miundombinu inaboreshwa kwa ufanisi.

About The Author

error: Content is protected !!