January 18, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

CBE yajivunia mafanikio lukuki miaka 60 ya uhai wake

 

NAIBU Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) yanayotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa wiki ijayo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, alisema kuwa CBE iliyoanzishwa mwaka 1965, kufuatia makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali za Tanzania na Ujerumani imekuwa na mafanikio makubwa.

Alisema maadhimisho hayo yatafanyika katika viwanja vya kampasi kuu hapa Dar es Salaam, ambapo wanatarajia kuwa maadhimisho hayo yatahudhuriwa na watu 300.

Profesa Lwoga alisema maadhimisho hayo yataambatana na shughuli nyingine mbalimbambali ikiwemo kusaini hati za makubaliano kati ya Chuo na wadau mbalimbali, uzinduzi wa Dira ya Miaka 50 ya Chuo, Ugawaji zawadi kwa watu maalum, kukata cake pamoja na burudani.

Kuhusu mafanikio ya Chuo katika kipindi cha Miaka 60, Profesa Lwoga alisema tangu kifunguliwe rasmi na Rais wa kwanza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, CBE imekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa elimu bora ya biashara, kukua na kuboresha huduma zake kuendana na mahitaji ya soko.

Alitaja maeneo yaliyoboreshwa kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya kampasi na wanafunzi ambapo Chuo kilianza na Kampasi moja ya Dar es salaam na idadi ya wanafunzi 30 tu ambapo hivi sasa kina Kampasi nne na idadi ya wanafunzi imeongezeka maradufu.

Alisema kwa sasa kampasi ya Dar es salaam ina wanafunzi wanafunzi 14,536, Dodoma iliyoanzishwa mwaka 1983 ina wanafunzi 4,611, Mwanza ilianzishwa 2007 idadi ya wanafunzi 2,098 na Mbeya ilianzishwa 2013 ina wanafunzi 1018 na kwamba hiyo inafanya jumla ya wanafunzi kwa Chuo kizima kufikia 22,263.

Kuhusu idadi ya Programu, Profesa Lwoga alisema chuo u kimepanua programu zake kutoka katika ngazi ya Astashahada hadi ngazi ya Shahada za Uzamili ambapo hivi sasa chuo kinatoa jumla ya programu 63.

Alisema CBE imejenga ushirikiano na taasisi za Kitaifa na Kimataifa ili kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinakuwa za ubora wa hali ya juu na zenye ushawishi mkubwa ambapo katika kipindi cha miaka 5 jumla ya machapisho 288 yametoka katika majarida ya Kitaifa na Kimataifa.

Alisema Chuo kina jumla ya watumishi 499, ambapo 482 ni wa kudumu na 17 wapo katika mkatab na kwamba Kati ya watumishi 499 watumishi 244 ni wahadhiri, na 251 watumishi waendeshaji.

“Kwa ujumla, mafanikio haya katika taaluma na tafiti yanathibitisha kuwa CBE ni kiongozi katika kuimarisha elimu ya biashara na kukuza maarifa yenye tija kwa maendeleo ya taifa. Chuo kinaendelea kuwekeza katika masomo ya ubunifu na tafiti zenye lengo la kujenga uchumi endelevu wa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema.

About The Author

error: Content is protected !!