December 11, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Hatua tano za kukamilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -Mipango na Maendeleo, Prof. Kitila Mkumbo

 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ametangaza hatua muhimu zinazofuata katika mchakato wa kukamilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 baada ya uzinduzi wa Rasimu ya Kwanza ya Dira hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Uzinduzi huo unafanyika Zanzibar tarehe 11 Desemba 2024, ukiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Kitila amebainisha kuwa mchakato wa kukamilisha Dira ya Taifa utapitia hatua tano muhimu zinazolenga kukusanya maoni zaidi ya wananchi, kuyahakiki, na kuyajumuisha kwenye Dira. Hatua hizo zitahusisha maoni ya wananchi na wadau mbalimbali, mijadala ya vyombo vya serikali, na hatimaye mjadala wa bunge kabla ya Dira hiyo kuidhinishwa rasmi.

Kwa mujibu wa Profesa Kitila, maoni mapya yataanza kukusanywa tarehe 14 Desemba 2024 kupitia hatua ya uhakiki ya Rasimu ya Dira. Shughuli hii itahitimishwa tarehe 14 Januari 2025, ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, atapokea Rasimu ya Pili iliyoboreshwa.

Baada ya hapo, maamuzi ya serikali yatafanyika kupitia Makatibu Wakuu, Tume ya Taifa ya Mipango, na Baraza la Mawaziri. Hatua ya mwisho ya mchakato huu itakuwa kuwasilisha Rasimu hiyo Bungeni kati ya Aprili na Mei 2025 kwa ajili ya majadiliano na uidhinishaji rasmi.

Hatimaye, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuzindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kati ya Mei na Juni 2025, kulingana na ratiba yake.

Profesa Kitila amesisitiza kuwa dira hiyo ni mali ya wananchi, na mchakato mzima unalenga kuhusisha maoni yao kwa kiwango kikubwa, kuhakikisha kuwa ndoto za maendeleo ya nchi zinazingatia matamanio na matarajio ya makundi yote ya jamii.

About The Author

error: Content is protected !!