MKAGUZI maarufu wa mahesabu hapa nchini, Yona Hezekiah Malundo kupitia kampuni yake ya Y.H Malundo na wenzake wanne wametunukiwa udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Read Impact kilichopo Colorado nchini Marekani. Anaripoti Makuburi Ally, Dar es Salaam … (endelea).
Tukio hilo la heshima lilifanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa Tanganyika 2 ulioko kwenye hoteli ya Land Mark Ubungo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.
Kwa tukio hilo, Tanzania imepokea heshima ya aina yake kwa watanzania kwa sababu ya umahiri wa walioonesha.
Akizungumza katika hafla hiyo mwakilishi wa Chuo hicho, Askofu Dk. Peter Rashid Abubakar alisema tuzo hizo zimetokana na uwasilishaji wa CV zao kwa chuo hicho.
Dk Rashid alisema baada ya kukabidhiwa vyeti hivyo hivi karibuni watakabidhiwa vyeti vya utambulisho kutoka katika chuo hicho ili waendeleze gurudumu la maendeleo ya Taifa.
“Tuzo zilizopokelewa ni heshima kwao na Taifa kwa ujumla, kinachotakiwa ni utekelezaji wa majukumu inavyotakikana ndani na nje ya nchi,” alisema.
Dk Rashid ambaye ndiye mratibu wa chuo hicho kwa nchi tano ikiwemo Tanzania, Rwanda, Uganda na nyinginezo, aliwapongeza waliotunukiwa udaktari huo kwamba wamefanya kazi zao inavyotakiwa ambako anatumia fursa hiyo kuiasa jamii kuandaa CV zao ili waweze kutunukiwa udaktari na chuo hicho.
Chuo hicho msingi wake ni dini na kueleza kwamba udaktari huo wa heshima ni kazi zao zimeonekana katika jamii.
Alisema kwa kuwa yeye ni mhadhiri wa tawi la chuo hicho hapa nchini anatoa wito kwa vijana kujiandaa ili kifunguliwe chuo hicho hapa nchini.
Wengine waliotunukiwa vyeti vya udaktari wa heshima ni Mkurugenzi Mkuu Jenga Africa Empowering Society Build Nation (ESBN), Dk Paul Kanijo, Mkurugenzi wa Mesodate Consultants ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Millenium Solution Development Trust Fund, Dk Emmanuel Jeremiah.
Wengine ni Dk Boniface Mbelwa na mkewe Dk Chriatian Robert Mbelwa ambao ni mke na mume.
Aidha naye Diwani wa Viti Maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Juliet Banigwa aliwapongeza madaktari wenzake kwa tuzo hizo za udaktari sambamba na kumshukuru Dk Rashid.
Dk Juliet alisema tuzo hizo ni furaha na heshima kubwa kwa nchi kwani wataendelea kuwainua na kuwaimarisha watu na jamii kwa ujumla.
Dk Malundo alisema udaktari aliotunukiwa atautumia kwa wasiojiweza kwa sababu ndio eneo lake kuwasaidia wenye uhitaji.
Mkurugenzi wa Jenga Africa, Dk Kanijo alimshukuru Mungu kwa sababu wamesimama muda mrefu kuitumikia jamii.
Dk Kanijo alisema tuzo hizo ni jambo jema na baraka ambako anajisikia fahari na wataongeza jitihada zaidi katika utekelezaji wa majukumu.
Dk Jeremiah alisema watatekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi ili kuimarisha ujenzi wa Taifa.
ZINAZOFANANA
Wanafunzi Tusiime waanza ziara nchini Uturuki
‘CODE LIKE A GIRL’ imewajengea uwezo wa Tehama wasichana Dodoma
Tanzania yaandika historia: Wanafunzi wa Arusha Science wapata ushindi wa kimataifa