January 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

SBL yapaisha viwango vya ukarimu Tanzania kufikia viwango vya Kimataifa

WANAFUNZI wanaosomea fani ya ukarimu katika Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) sasa watapata mafunzo ya ziada ya miezi mitatu kutoka kwa watalaamu wa Serengeti Breweries Limited (SBL) huku kampuni hii ikilenga kusaidia kujenga kizazi kipya cha wataalamu wa sekta ya utalii na ukarimu inayokua kwa kasi nchini Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kupitia makubaliano yaliyosainiwa mwezi Septemba kati ya chuo hicho na SBL, kundi la kwanza la wanafunzi zaidi ya 100 tayari wamejiunga na mpango huu kama sehemu ya mpango wa mafunzo ya ujuzi wa maisha uitwao “Skills for Life”.

Wanafunzi hawa watajifunza miongoni mwa mambo mengine, viwango vya kimataifa vya utoaji wa vinywaji vya pombe ikiwa ni pamoja na ustadi wa kutengeneza mchanganyiko wa vinywaji vilivyo (cocktails) na visivyo na kilevi (mocktails) pamoja na kuboresha viwango vya huduma za baa na vinywaji.

Haya ni mafunzo ya kipekee yanayoenda mbali na ujuzi wa kiufundi na kutoa mafunzo ya ujuzi wa maisha kama vile kutengeneza chapa binafsi, usimamizi wa muda, uongozi, na ufanisi katika mawasiliano,” alisema Rispa Hatibu wakati wa hafla ya ufunguzi wa kundi hilo la kwanza la wanafunzi.

Hatibu, ambaye ni Meneja Mawasiliano na Uendelevu wa SBL, alisisitiza dhamira ya kampuni katika maendeleo ya vijana akisema, “Mpango huu ni zaidi ya ujuzi tu—ni kuhusu kuwawezesha vijana na zana za kubadilisha maisha yao na kusaidia ukuaji wa sekta ya utalii na ukarimu nchini.”

Kwa upande wake, Mary Maduhu ambaye ni Meneja wa Taaluma kutoka NCT alielezea programu hii kama ishara ya maono ya ushirikiano kati ya SBL na NCT. “Mafunzo haya siyo tu yanahusu ujuzi wa kiufundi; ni kuhusu kufungua uwezo na kuhamasisha vipaji kwa wanafunzi. Pia ni mwanzo wa safari kuelekea ukuaji wa kitaaluma na kibinafsi,” alisema Maduhu.

Aliongeza kuwa sekta ya utalii ya Tanzania inakua kwa kasi na hivyo kuongeza mahitaji ya nguvu kazi yenye ujuzi wa sekta hiyo, pengo ambalo alisema ushirikiano kati ya SBL na NCT utasaidia kulijaza kwa kutengeneza nguvu kazi inayokidhi viwango vya kimataifa vya ukarimu.

Zaidi ya athari yake ya moja kwa moja kwa wanafunzi, programu hii pia inaashiria dhamira pana kwa maendeleo endelevu. Kwa kukuza talanta na kuongeza ajira, SBL na NCT wanachangia katika ukuaji wa kijamii na kiuchumi wa taifa la Tanzania,” aliongeza Mkuu huyo wa Taaluma.

About The Author

error: Content is protected !!