SHIRIKA La Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limezindua programu yake ya elimu endelevu inayoitwa “Vijana kwa Utekelezaji wa Mabadiliko ya Tabianchi,” ambayo inalenga kutoa elimu na uelewa kwa watoto na vijana ili washiriki kikamilifu katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi visiwani Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Akizungumza na washiriki , maafisa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Chunga na Sekondari ya Tumekuja jana, Mwakilishi Mkazi wa UNICEF, Laxmi Bhawami alisema kuwa mabadiliko ya tabianchi yana athari nyingi kwa maisha ya binadamu kama vile kuzidi kwa joto kali na mabadiliko mengine ya kimazingira yanayoleta athari mbaya kwa magonjwa hasa watoto.
“Tunawatumia watoto kushiriki katika juhudi hizi za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa sababu ni bora kuwafundisha na kuwapa uelewa na maarifa kuhusu ongezeko la joto la kidunia ili vijana waanze kujua mbinu mbadala za kuzuia mabadiliko ya tabianchi kuanzia ngazi ya msingi,” alisema.
Bi Bhawami alibainisha kuwa mabadiliko ya tabianchi, pamoja na mambo mengine mabadiliko haya yanaweza kusababisha ukame, kupunguza uzalishaji wa chakula kwenye kilimo na kutishia usalama wa chakula duniani kote.
Alisema kwamba moja ya athari za mabadiliko ya tabianchi katika kisiwa hicho ni kuongezeka kwa kiwango usawa wa bahari, kupanda kwa joto, kubadilika kwa mtindo wa maisha pamoja na kusababisha ueneaji wa magonjwa kama malaria kutokana na mafuriko na kuweka jamii katika hatari magonjwa ya mlipuko.
“Hivyo, tunawawezesha na kuwapa vijana maarifa, elimu na taarifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na njia bora za kupunguza tatizo hili katika siku zijazo,” alifafanua Bhawami.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amani, Bi Asya Iddi Issa alisema kuwa programu ya kupanda miti inapaswa kuwa endelevu kwa kuimwagilia na kutunza miti hiyo ili kuleta hewa safi, matunda na kivuli pamoja na mambo mengine kuweka mazingira safi na salama.
Aliongeza kwamba ni muhimu programu hiyo ikaendelea kwa vitendo kwa kuunda vilabu na madarasa ya kujifunza namna bora ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi katika ngazi za chini mpaka taifa kwa kuwajengea uwezo Watoto na vijana hapa nchini.
“Vilabu vya Watoto na vijana jinsi ya kupambana na mabadiliko tabianchini ni muhimu kupewa kipaumbele cha kipekee na nawapongeza UNICEF kwa kuanzisha program hii na zoezi hili la upandaji miti, nataka liende mpaka kwenye mitaa hapa Zanzibar,”
“Haya masuala ya mabadiliko ya tabianchi, tunapaswa kuongeza mijadala katika mitaa, vijini, vitongoji ili jamii nzima na vijana wetu wachukue hatua kuhusu athari hizi na umuhimu wa kupanda miti kama sehemu ya juhudi za kupunguza tishio hili kwa jamii yetu ,” alieleza.
Kwa upande wake, Afisa wa UNICEF Maji na Mazingira, Marko Msambazi alisema kwamba programu hii inazingatia jinsi ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kiufundi wa kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi katika maisha yao kila siku.
“Tumepanda miti leo katika Shule ya Msingi ya Chunga katika Mkoa Mjini Magharibi na kuonyesha kwa vitendo jinsi ya kupanda miti kwa umuhimu kupata oksijeni na mambo mengine muhimu yanayochangia maendeleo ya kijamii pamoja na kutunza mazingira,” alieleza.
Alisema kwamba mbali na kupanda miti, pia shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto ina programu ya kuchakata taka kama vile mifuko ya plastiki na taka zingine kama mbadala wa kutengeneza bidhaa mbalimbali na kupunguza tatizo la ajira.
Balozi wa Mazingira , Nasra Khatibu Abdallah , mwanafunzi wa kidato cha sita kutoka shule ya Sekondari Bembela, ambaye alishiriki mkutano wa mabadiliko ya tabianchi (COP29) nchini Uzbekistan alisema ni muhimu kwa wadau wote kushiriki kikamilifu katika juhudi za kupunguza mabadiliko ya tabianchini.
“athari za mabadiliko ya tabianchini ni kubwa sana kwa Watoto na vijana mashuleni katika maeneo ya kusomea na zoezi la leo la upandaji miti liwe endelevu ili kupunguza joto na kuweka mazingira safi kwa Watoto kusoma,’ alisema
Programu hiyo ambayo iliendana sambamba na zoezi la upandaji miti ili kuweza kupunguza joto, upande hewa safi na matunda ilikuwa ni moja ya agenda ya shirika hilo katika kusambaza elimu na taarifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabiachi.
ZINAZOFANANA
Shangwe la Mwaka Mpya 2025: Bei za mafuta zaendelea kushuka
Bilioni 3 zatinga mfukoni madawa
CCM yampongeza Mkurugenzi wa shule za Tusiime