MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango amesema katika kumuenzi Jenerali Mstaafu David Musuguri inapaswa Watanzania wote yaani askari na raia kujitoa, hata ikibidi kufa kwa ajili ya kulinda na kutetea uhuru, heshima na maslahi ya Taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa kuaga mwili wa Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali David Bugozi Musuguri katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo Jijini Dar es salaam. Ametoa rai hasa kwa vijana wa Tanzania kuipenda nchi na jeshi la Tanzania kwa moyo wote na kuwa tayari kuilinda Tanzania kwa gharama yoyote kama alivyofanya Jenerali (Mstaafu) Musuguri.
Makamu wa Rais amesema Makamanda na Wapiganaji waliopewa dhamana ya uongozi katika Jeshi hawana budi kuendelea kufuata mfano bora uliyoachwa na Jenerali Mstaafu David Musuguri.
Amesema Hayati Jenerali (Mstaafu) Musuguri alilipenda sana Jeshi maisha yake yote. Alitamani vijana wengi wajiunge na Jeshi na alifanikiwa sana kuwaandikisha jeshini vijana wengi. Amesema alikuwa mwalimu na mlezi makini wa askari vijana.
Aidha, alipopewa jukumu la kuongoza Jeshi la Wananchi wa Tanzania alifanya jitihada kubwa kulijenga na kuliendeleza Jeshi na kulifanya kuwa kati ya Majeshi bora na imara barani Afrika ndiyo maana Jeshi la Idd Amin lilipovamia kipande cha ardhi ya Tanzania lilidhibitiwa kutoka kwa Jeshi la Tanzania likiongozwa na Jenerali Mstaafu Musuguri.
Makamu wa Rais ametoa salamu za pole Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali nzima kwa Mkuu wa Majeshi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa ujumla, familia, ndugu wa Marehemu na Watanzania wote kwa msiba huu mkubwa kwa Taifa. Amesema Serikali inaiombea faraja familia ya hayati Musuguri na wote walioguswa na msiba huu na kuwahakikishia kwamba Serikali na Taifa zima ipo pamoja nao.
ZINAZOFANANA
Rostam ataka wakopeshaji wakubwa duniani kuipunguzia Afrika riba
TMA yatoa utabiri wa mvua za msimu wa Novemba 2024 hadi Aprili 2025
Wafugaji watamba kuwaweka viongozi wa wilaya mfukoni