December 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Rostam ataka wakopeshaji wakubwa duniani kuipunguzia Afrika riba

Rostam Azizi

 

Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, ametoa wito kwa mashirika makubwa ya kifedha duniani kupunguza riba za mikopo kwa Afrika ili ziwe sawa na zile zinazotolewa kwa mataifa ya Ulaya, Marekani, na Asia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Rostam alisema hayo jana jijini London wakati aliposhiriki kwenye majadiliano katika Mkutano wa kimataifa wa Financial Times Africa Summit uliofanyika kwa siku mbili, Oktoba 29 na 30.

Mkutano wa FT Africa Summit ulihudhuriwa na wakuu wa nchi, Magavana wa Mabenki Kuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Mawaziri wa Uingereza, pamoja na wawakilishi wa IMF, Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa, mabenki na wadau wengine muhimu.

Akizungumza katika mkutano huo ambao ndiyo ndiyo kusanyuko la juu kabisa kimataifa kuzungumzia mikakati ya uwekezaji barani Afrika, Rostam alisema kuwa uamuzi wa kuzipunguzia riba nchi za Afrika ni wa msingi kwa sababu takwimu zinaonyesha ndizo zilizo na kiwango kidogo sana cha kutolipa mikopo ikilinganishwa na mataifa mengine.

Akitoa takwimu, Rostam alisema kuwa kati ya makampuni yapatayo 800 duniani yaliyotoa mikopo kwa mwaka 2021, kiwango cha kutolipa mikopo (default rate) kwa nchi za Afrika kilikuwa chini ya asilimia mbili, wakati kwa nchi za Ulaya kilikuwa zaidi ya asilimia tano, kwa mataifa ya Marekani Kusini (Latin America) karibu asilimia 12, na kwa Marekani ilikuwa karibu asilimia sita.

Alisema licha ya takwimu hizi, bado Afrika inaadhibiwa kwa namna isiyo ya haki kwa kutozwa riba kubwa, akiita hali hii kuwa yenye utata (paradox) usioelezeka.

Pia, Rostam alizitaka nchi tajiri katika kundi la G7 kutunga sera zitakazozilazimisha benki kutenga mgao maalum wa mikopo kwa ajili ya Afrika.

Rostam alisema, “Afrika inahitaji fursa sawa na nafuu ya kupata fedha kwa kiwango kikubwa ili kukidhi mahitaji yake ya maendeleo.”

Aliendelea na kuzikosoa taasisi za upimaji viwango vya mikopo, akisema kuwa zinafanya makosa ya kuzipa baadhi ya nchi za Amerika Kusini alama za juu zaidi za mikopo kuliko nchi za Afrika, hata kama hali yao ya kiuchumi ni sawa.

Pia alihoji juu ya viwango vya riba visivyo sawa, akisema kuwa nchi ya Afrika yenye vigezo ya mkopo sawa na na vya nchi ya Amerika Kusini, Ulaya Mashariki au Asia bado inatozwa riba kubwa zaidi.

Akitoa mfano alisema kuwa Ufilipino au Iraq zinapata viwango vya riba vya chini kuliko Botswana, ambayo japo ipo Afrika uchumi wake una mazingira yanayovutia uwekezaji kwa kiwango kile kile cha mataifa ya Ulaya.

Kwa mujibu wa Rostam, kuna makosa katika uwekaji wa viwango vya ya riba kwa Afrika kutoka kwa wakopeshaji wakubwa wa kimataifa, hali ambayo inahitaji hatua za haraka kuchukuliwa sasa hivi ili kumaliza kasoro hii.

About The Author

error: Content is protected !!