WAFANYABIASHARA wanaopewa zabuni za ujenzi wa miradi ya Serikali wilayani Liwale, wamesusa kazi hizo baada ya wakandarasi wengi kudhulumiwa mamilioni ya fedha za kazi wanazofanya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Liwale, Lindi … (endelea).
Taarifa zinaeleza kuwa pamoja na mabilioni ya fedha yanayotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya miradi ya maendeleo wilayani humo, wazabuni wa kazi hizo hawalipwi na badala yake zinaishia mikononi mwa wajanja wachache
Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Halmashauri hiyo unalazimika kutumia wazabuni wa nje ya wilaya kuwapa kazi kwa zabuni zilizosusiwa na wafanyabiashara wa eneo hilo.
Akizungumza na Gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara hao, Yassin Manuu alisema Halmashauri hiyo inawafanya wao kama watu wasio na elimu, kwani licha ya kukamilisha miradi ya zabuni wanazopewa, wamekuwa hawalipwi fedha zao.
Aliongeza, kuwa sababu inayotumiwa na baadhi ya watendaji wa Serikali kutolipa fedha zao ni madai kuwa mikataba waliyoingia ina makosa kisheria.
“Ni mambo ya ajabu sana, wanaotuingiza kwenye mikataba ni hao hao watendaji wa Serikali, unapofuatilia malipo, unaambiwa uliingia mkataba wa maneno au hukufuata utaratibu, sasa unashangaa kwa nini sikuambiwa kasoro hizo mapema?” Alihoji Yassin na kuongeza:
“Sisi ni chama cha wafanyabiashara na ndio wazabuni wa kazi za miradi ya Serikali. Wapo waliopewa kazi za ujenzi, wakakopa fedha benki, wakakamilisha, lakini fedha hawalipwi, hali hiyo imekuwa ikituweka kwenye wakati mgumu sana, ndiyo maana sasa hakuna aliye tayari kufanya kazi za Serikali,” alisema.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, Serikali ya Rais Samia hivi sasa imepeleka mabilioni ya fedha za miradi, lakini hakuna mfanyabiashara aliye tayari kuomba zabuni kutokana na dhuluma hiyo.
Aliongeza, kuwa kibaya zaidi baadhi ya watendaji walioingia mikataba na wazabuni na kushindwa kuwalipa, bado wapo kazini na wengine wamehamia wilaya jirani, wakiendelea kutamba bila kuchukuliwa hatua.
“Hapa wilayani, kuna wafanyabiashara zaidi ya 15 wamefanya kazi kubwa za Serikali kwa kukopa benki, lakini hawajalipwa. Hao ndugu zetu wana wakati mgumu sana, maana wako kwenye hatari ya kuuziwa mali zao.
“Tunamwomba Rais Samia Suluhu Hassan, aingilie kati uonevu huo na watumishi waliokula fedha hizo, wachukuliwe hatua,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Godluck Mringa alikiri kuwa alipohamishiwa hapo, alikuta tatizo hilo na ni kubwa na anaendelea kukabiliana nalo.
Alisema hadi sasa uhusiano kati ya wafanyabiashara na Serikali si mzuri kutokana na migogoro hiyo ya kutolipa fedha za watu.
“Ni jambo gumu na baya sana, hivi sasa nikitaka kuchangisha fedha kutoka kwa wafanyabiashara kwa jambo lolote la maendeleo wilayani hapa, sipati hata Sh milioni tano.
“Hili si jambo jema kwa kweli, na nimetoa maelekezo kwa Mkurugenzi kwamba kuanzia sasa, mambo hayo yabaki kuwa historia chini ya uongozi wangu,” alisema Mringa.
Alisisitiza kuendelea kupigania maslahi ya wazabuni hao, lakini kuanzia sasa mtumishi akatayezingua kwenye kuwalipa, atazinguana naye.
ZINAZOFANANA
Benki ya NBC yatambulisha kampeni ya Kilimo Mahususi kwa wakulima na wafugaji Mbeya
Upelelezi wakwamisha kesi ya Boni Yai
Wahitimu 417 kutunikiwa vyetu ITA