WATAALAM 544 wa kada ya afya, katika nyanja ya sita ikiwamo ya watoto wachanga, afya ya akili, magonjwa yasiyoambukiza kama ya moyo na matibabu ya ubongo na mishipa ya fahamu, wametengewa Sh. 14 bilioni kujiendeleza kielimu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Aidha, nyanja nyingine ni ugunduzi wa magonjwa ikiwamo patholojia, huduma za utengamao na tiba shufaa.
Waziri wa Afya, Jenister Mhagama, ameyasema hayo mjini Dodoma leo tarehe 21 Oktoba 2024, alipozungumza na waandishi wa habari.
Amesema fedha hizo zimetengwa katika mwaka huu wa fedha 2024/2025, zikiwa na ongezeko la Sh. 3.05 bilioni (sawa na asilimia 28), zilizotengwa kufadhili masomo ya wataalamu hao, mwaka 2023/2024.
“Fedha hizi zitatumika kugharamia mafunzo kwa wataalamu wapya 544 kwa mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi, pamoja na wataalamu wengine 47 kwa utaratibu wa seti. Wataalamu 829 wanaoendelea na masomo ya ubingwa na ubobezi katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi, wataendelea kupewa ufadhili kupitia fedha hizo,” amesema.
Amesema asilimia 95 ya waombaji hao wamepata ufadhili katika vyuo vya ndani na asilimia tano watasoma nje ya nchi.
Mhagama amesema ufadhili unatolewa chini ya utaratibu wa mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan, wa kuongeza wataalamu bingwa na bobezi wa afya nchini (Samia Health Specialization Scholarship Program 2024/25).
“Kipaumbele kimetolewa kwa watumishi wanaofanya kazi kwenye maeneo yenye uhaba mkubwa wa wataalamu bingwa kwa kuzingatia uwiano wa kijiografia…napenda kuwatangazia watumishi wote waliopata ufadhili kwa mwaka 2024/2025, kwamba wanapaswa kukamilisha taratibu za kujaza mikataba ya ufadhili kama kigezo cha kukubali ufadhili huu kabla ya tarehe 01 Novemba 2024,” amesema.
Amesema lengo la serikali ni kufanya mageuzi katika sekta ya afya, ili wananchi wapate huduma bora za matibabu hasa ya kibingwa na ubingwa bobezi hapa nchini.
Amesema lengo lingine ni kufanikisha tiba utalii kwa kuongeza wataalamu pamoja na vifaa tiba, ikiwa ni utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano (2020-2025) wa wizara hiyo, kusomesha wataalamu bingwa na wabobezi wasiopungua 300 kwa kila mwaka wa fedha.
“Jitihada hizo zimelenga kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, kupunguza rufaa za matibabu nje ya nchi na hivyo kupunguza gharama kwa Serikali na wananchi pamoja na kuvutia tiba utalii,” amesema Mhagama.
Waziri Mhagama amesema ufadhili unajumuisha ada ya mafunzo na posho ya utafiti kwa watakaofadhiliwa ndani ya nchi, wakati watakaoenda kusoma vyuo vya nje ya nchi watalipiwa ada, posho ya kujikimu wakiwa masomoni, nauli ya kwenda na kurudi pamoja na posho ya utafiti.
ZINAZOFANANA
Wakazi wa Mdundwaro waishukuru TASAF kuwajengea nyumba ya watumishi
Madaktari wa Tanzania wahitimisha Kambi tiba Comoro kwa ufanisi mkubwa
Wananchi Comoro wafurahia huduma madaktari wakitanzania