October 18, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Kada nne za afya zatungiwa mitaala mipya

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel

 

Serikali ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mitaala mipya ya kada ya Uuguzi, Ukunga, Famasia na Fiziotherapia, itakayoanza kutumika mwaka ujao wa masomo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, ameyasema hayo leo Oktoba 18, 2024 kwenye kikao kilichozikutanisha kwa pamoja Kamati ya Bunge za Afya na Masuala ya Ukimwi pamoja na Kamati ya Elimu, Utamaduni na Michezo na Viongozi na Wataalam kutoka Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu.

Dk. Mollel ambaye amezungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, amesema Serikali itaendelea kuwashirikisha na kuwaelimisha wadau katika hatua mbalimbali za usimamizi na uendeshaji wa mafunzo kwa maslahi mapana ya Taifa, ili kulinda na kuboresha huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi.

“Katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, itaandaa vikao vya wadau wa mitaala ya mafunzo kwa kila mtaala ili kupata maoni yao yatakayosaidia kufanya maboresho ya mitaala hiyo,” amesema Dk. Mollel.

Dk. Mollel amebainisha kuwa Wizara imejipanga kusambaza mitaala mipya iliyohuishwa kuanzia Julai hadi Septemba mwakani, ili ianze kutumika kwenye mwaka wa masomo 2025/2026, utakaoanza Oktoba 2025.

Nazo Kamati za Kudumu za Bunge zinazohusika na masuala ya afya na elimu, zimetoa rai kwa Serikali kushirikiana na wadau wa kisekta katika kuboresha mitaala mipya ya kada hizo.

Kamati hizo zimeshauri Wizara ya Afya kushirikiana na Wadau kwa kuzingatia kanuni, taratibu za mabaraza za uandaaji wa mitaala.

Aidha, Kamati imeitaka Wizara ya Afya kuandaa vikao vya kuwaelimisha wadau, kuhusu uhusiano uliopo baina ya vigezo na maudhui yaliyopendekezwa kwenye mitaala.

About The Author