December 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Gambo alia na soko la Tanzanite, amuomba Rais Samia aingilie kati

 

MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini Mrisho Gambo, amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati suala la biashara ya madini ya Tanzanite kwa kuyaruhusu kuuzwa katika masoko yote ya madini nchi nzima, ili rasilimali hiyo ya Taifa iweze kuwanufaisha watanzania wote. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Hayo yamezungumzwa leo tarehe 18 Oktoba, 2024, katika mkutano baina ya Mbunge Gambo na Brokers/wafanyabiashara wadogo wa madini Arusha ambao wametoa hisia zao mbele ya mbunge huyo wakionyesha kutoridhika na madini ya Tanzanite kuuzwa kama madawa ya kulevya.

“Nina imani kubwa na Rais Samia kwani ni kiongozi mpenda haki , anaamini kwenye biashara huria na anayependa watanzania wanufaike na rasilimali zao , hivyo hata katika suala la madini ya Tanzanite kuuzwa katika soko huru atashughulika nalo” amesema Mbunge Gambo.

Gambo amesema Madini ya Tanzanite ni madini yenye jina kubwa duniani cha kushangaza madini ya kutoka nchini DRC Congo yapo katika soko la madini mkoa wa Arusha lakini Tanzanite inayochimbwa katika mji wa Mererani mkoani Manyara haiwezi kuuzwa katika soko hilo mkoani humo.

Amesema toka kuasisiwa kwa katazo la madini hayo kuuzwa kiholela, thamani yake imezidi kuporomoka kwani kwa mujibu wa takwimu kutoka tume ya madini, mwaka 2017 – 2018 gramu 476,000 thamani yake ilikuwa Sh. 55 bilioni na mwaka 2022 – 2023 gramu 23,000,015 thamani yake ni Sh. 56 bilioni jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa kumekuwepo na anguko kubwa la bei ya madini hayo adimu duniani.

“Mnaweza mkaona kabisa hawa ambao wanataka kuyafungia madini ya Tanzanite wanalipeleka wapi taifa, kwa hiyo hili jambo kwani ni jambo very serious hatuangalii ajira peke yake, siku za nyuma ukiacha hawa mabroker hapa pale kwenye jengo la PSSF lilikuwa limejaa, kulikuwa na mashine za kutosha watu wanakata madini leo hakuna kitu” amesema Gambo.

Ameongeza” Huyo mtu anayewashinikiza na kulifanya taifa lipate hasara lazima kumtafakari, kwa sababu lazima tuache ubinafsi, taifa linapata hasara nchi inapata hasara kwa sababu ya ubinafsi”

Gambo amesema kutokutoa uhuru wa kufanya biashara hiyo na kutengeneza sheria ambazo hazimlindi mfanyabiashara mdogo wa kati na mkubwa, kunasababisha utorishaji wa madini hayo kwa njia ya panya, kuongezeka kwa ujanja ujanja pamoja na kuibuka kwa makundi ya ubabaishaji yasiyokuwa na lengo jema la kuyalinda madini hayo kwa wivu mkubwa.

“Basi mmepractise mlichokuwa mnakiona, mmepata hasara, maana mngepata faida mngesema maana inawezekana huko zamani mlizani kwamba biashara hii mauzo yanakuwa madogo kwa sababu madini yanauzwa kiholela, leo mmeyadhibiti kwenye ukuta huko merereni yameshuka kuliko huko nyuma ilivyokuwa” Amesema Mbunge Gambo.

Amesema duniani kote biashara ya madini hufanyika kwa watu kuchimba madini eneo husika na kwenda kuyauza sehemu nyingine, tofauti na madini ya Tanzanite ambapo yanachimbwa eneo moja na biashara ya kuyauza inafanyia katika eneo hilohilo la mgodi.

Mbunge Gambo amesema furaha yake ni kuona madini ya Tanzanite yanauzwa nchi nzima bila kuwekewa vikwazo, kwani baada ya Serikali kutatua suala la Leseni halitamsaidia mfanyabiashara kwani atakosa madini ya kuuzwa kutokana na zuio ama katazo lililopo linalotaka madini hayo kununuliwa Mererani na kuuzwa nje ya nchi pekee.

“Kama jinsi mlima kilimanjaro sio wa watu wa mkoa wa Kilimanjaro bali ni wa nchi nzima kadhalika tunatamani madini haya yasiwe ya watu wa upande fulani tu bali yauzwe nchi nzima ili yaweze kuwanufaisha watanzania wote,” amesema Mbunge Gambo.

About The Author

error: Content is protected !!