MKURUGENZI wa Huduma za Tiba Dk. Hamad Nyembea, amewataka wazazi na walezi, kulinda afya ya macho ya watoto, kwa kuzingatia muda wanaotumia kwenye runinga, simu pamoja na kompyuta. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Dk. Nyembea ameyasema hayo leo tarehe 09 Oktoba 2024, alipokuwa akifunga maadhimisho ya wiki ya macho Duniani yaliyofanyika katika kituo cha Afya Makora jijini Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Jenista Mhagama.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Penda Macho yako, Muhamasishe Mtoto kupenda Macho yake.”
Amesema zaidi ya watu milioni 1.6 wamehudumiwa kwenye kliniki za kutoa huduma za macho kwa mwaka 2023, kati ya hao, asilimia 42 walikuwa na umri chini ya miaka 15, huku asilimia 6 ya watoto hao wakiwa wenye ulemavu wa kuona.
Dk. Nyembea amesema vyanzo vikubwa vya matatizo ya macho kwa watoto na vijana ni mzio, upeo mdogo wa macho kuona unaorekebishika kwa miwani na majeraha kwenye macho.
Aidha, amesema matatizo ya macho yanaweza kusababishwa pia na mtoto wa jicho (asilimia 10), makengeza (asilimia 1.5), makovu kwenye kioo cha jicho (asilimia 1.1), na vidonda kwenye vioo vya jicho (asilimia 1.5), ugonjwa wa surua, upungufu wa vitamini A na saratani ya macho.
“Sababu hizi zote zinaweza kuepukika au kudhibitiwa endapo tutachukua hatua stahiki mapema,” amesema Dk. Nyembea.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imeimarisha huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali za Rufaa za Kanda ya KCMC -Moshi na Bugando -Mwanza, ambapo kwa mwaka 2023, watoto 631 sawa na asilimia 24.5 ya watu waliohudumiwa, walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho na kupatiwa miwani.
“Ili kupanua wigo, Serikali imeongeza huduma hizi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma, lengo likiwa ni kufikia angalau asilimia 50 ya wahitaji wote ifikapo mwaka 2030.
“Serikali imekuwa ikifanya pia kambi maalum za uchunguzi na matibabu ya kibingwa na ubingwa Bobezi ili kuongeza kasi katika kuwahudumia wananchi katika maeneo yao na kupunguza gharama za kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizi,” ameongeza Dk. Nyembea.
ZINAZOFANANA
Wanafunzi Tusiime waanza ziara nchini Uturuki
‘CODE LIKE A GIRL’ imewajengea uwezo wa Tehama wasichana Dodoma
Tanzania yaandika historia: Wanafunzi wa Arusha Science wapata ushindi wa kimataifa