November 12, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC yajivunia maboresho ya huduma kukidhi mahitaji ya wateja

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua maadhimisho ya mwezi wa huduma wa kwa wateja huku ikijivunia mafanikio mbalimbali ikiwemo maboresho makubwa ya huduma zake yanayolenga kukidhi mahitaji ya wateja wa benki hiyo (Customer satisfaction). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hafla fupi ya uzinduzi wa maadhimisho hayo imefanyika mapema leo, Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Dar es Salaam ikihusisha viongozi waandamizi wa benki hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Theobald Sabi, wafanyakazi pamoja na baadhi ya wateja wakiwemo wale waliohudumiwa na benki hiyo kwa zaidi ya kipindi cha miaka 30.

Akizungumzia maadhimisho hayo yenye kauli mbiu “Above and Beyond”, Sabi alisema bado benki hiyo itaendelea kubeba kauli mbiu isemayo “Tunakuthamini” ikiwa na lengo la kuelezea maboresho iliyoyafanya katika utoaji wa huduma zake kufutia utamaduni wake wa kutumia vema mwezi huo kwa kukusanya maoni ya wateja ili kuwahudumia vizuri zaidi kwa kubuni huduma zinazoendana na mahitaji yao ili kufikia matarajio yao.

“Ili kufanikisha adhima yetu ya msingi ya kuhakikisha tunakidhi mahitaji ya wateja wetu, Benki ya NBC tumeendelea kuwekeza katika kuongeza mtandao wa matawi na mawakala, kuwekeza katika mifumo ya kidijitali na kuboresha taratibu za utoaji huduma mbalimbali ikiwemo utoaji wa mikopo ili kuongeza tija’’ alisema Sabi huku akitolea mfano huduma ya mikopo ya wastaafu ambapo benki hiyo imeongeza ukomo wa umri wa mkopaji kutoka miaka 70 mpaka Miaka 80 huku muda wa mkopo huo ukioongezeka kutoka miaka 6 hadi 9.

Kwa mujibu wa Sabi mwaka huu pekee benki hiyo imefanya maboresho mbalimbali ya kihuduma ikiwemo kuongeza mtandao wa matawi mapya 9 na hivyo kutimiza jumla ya matawi 60 nchi nzima, kuongeza mtandao wa mawakala (NBC Wakala) ambao sasa wanafika zaidi ya 16,950 nchi nzima sambamba na kufanya maboresho katika huduma kwa njia ya simu za mkononi NBC Kiganjani na ile ya NBC Connect.

“Zaidi tumefanya maboresho makubwa kwenye Mfumo wa ulipaji wa malipo ya serikali kupitia mfumo wa GEPG unaowapa wateja wetu uwezo wa kufanya malipo ya Serikali na kulipia ankara zao kwa urahisi zaidi.’’ Aliongeza huku akitumia fursa hiyo pia kutambulisha huduma mpya ya “Self Service Account Opening” inayotoa fursa kwa wateja wateja wa benki hiyo wanaotumia huduma za NBC Kiganjani na Tovuti ya NBC kuweza kufungua akaunti wao wenyewe popote walipo.

Akizungumzia maboresho kwenye utoaji wa mikopo ya benki hiyo, Sabi alitaja uwepo wa maboresho makubwa kwenye vigezo tofauti vinavyotumika katika utoaji wa mikopo mbalimbali ya benki hiyo ikiwemo Mikopo ya Wastaafu, mikopo inayochukuliwa kwa Dhamana ya Hatifungani (BOND), Mikopo ya Nyumba (Mortgage) na mikopo ya kilimo na ufugaji lengo likiwa ni kuwezesha ufikiaji wa wadau wengi zaidi wa sekta hizo ili waweze kunufaika na huduma za benki hiyo.

“Kwa mfano, mbali na mikopo ya wastaafu ambapo kwa sasa kiasi cha juu cha mkopo hiyo kimeongezeka kutoka Sh50 Milioni mpaka Sh300 Milioni pia tumeboresha vigezo vya upatikanaji wa mikopo ya nyumba yaani “Mortage” ambapo sasa mteja anaweza kukopa mpaka kiasi cha Sh. 1 Bilioni kwa muda wa miaka 25. Zaidi tumefanya uwezeshaji mkubwa katika sekta ya Kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania wote ambapo tumetoa mikopo ya matrekta, Bima kwa Wakulima na kuanzisha Akaunti maalumu kwa ajili ya wafugaji.,” alitaja.

Wakizungumza kwenye hafla hiyo baadhi ya wateja wa muda mrefu wa benki hiyo walionyesha kuridhishwa na mabadiliko ya kihuduma yanayoendelea kufanywa na benki hiyo huku wakionesha kuguswa zaidi na hatua ya benki kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji wa mikopo mbalimbali kwa kuondoa vigezo ambavyo havikuwa rafiki kwa baadhi ya wananchi wakiwemo wastaafu na wale ambao hawapo katika sekta rasmi.

“Kwa sisi ambao tumehudumiwa na benki hii kwa zaidi ya miaka 30 sasa tumejionea mabadiliko makubwa yanayohusisha maboresho chanya ya huduma za benki ya NBC. Licha ya taasisi nyingi za fedha kutokuwa na vigezo rafiki katika utoaji wa mikopo kwa wastaafu ni faraja kwetu kuona kwamba NBC ndio kwanza wameongeza ukomo wa umri wa mkopaji kutoka Miaka70 mpaka Miaka 80’’

“Hatua hii faraja kwetu zaidi kwa kuwa ukomo wa miaka 70 uliokuwepo hapo awali ulikwamisha jitihada zetu za kujikwamua kiuchumi wakati ambao sisi binafsi tulihisi bado tuna nguvu na wajibu wa kuendesha shughuli zetu kiuchumi,’’ alisema Bw Francis Mfundo kauli ambayo iliungwa mkono na wateja wenzie, Asaa Simba pamoja nae Zuhura Maganga.

About The Author