November 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wanaomiliki silaha kinyemela waitwa polisi

 

JESHI la Polisi nchini, limewataka wamiliki wa silaha kinyume cha sheria, kuzisalimisha kabla ya tarehe 31 Oktoba 2024. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime, kwa umma leo imeeleza kuwa watakaojitokeza kuzisalimisha kwa hiari hawatashtakiwa.

Katika taarifa hiyo, Misime amesema msamaha huo ulitolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Yusuf Masauni, kwa tangazo namba 783, tarehe 30 Agosti 2024; na utekelezaji wake ulianza Septemba Mosi na utaisha mwisho wa mwezi huu.

“Msamaha huo umetolewa na Serikali, kwa lengo la kuhakikisha kuwa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria zinaondoshwa katika jamii, ili zisisababishe madhara kwa raia kama vile vifo, majeruhi, watu kuhama makazi (wakimbizi wa ndani), njaa pamoja na uchumi kuzorota,” amesema.

Amesema wenye silaha hizo wanaweza kuzisalimisha katika vituo vya Polisi, Ofisi za Serikali za Mitaa na katika Ofisi za Watendaji Kata au Shehia, kila siku kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.

Amesema silaha zinazopaswa kusalimishwa, ni zile ambazo hazijawahi kusajiliwa hapa nchini na zimekuwa zikimilikiwa kinyume cha Sheria pamoja na zinazomilikiwa na ndugu wa marehemu baada ya mmiliki halali kufariki dunia.

“Silaha nyingine ni pamoja na ambazo ziko katika kundi la silaha za Kijeshi (assault rifles) kama vile AK47, G3, SKS, silaha ambazo zimetengenezwa kienyeji (homemade guns/craft arms/magobore) pamoja na aina yoyote ya mlipuko au risasi zinazomilikiwa kinyume cha Sheria,” amefafanua Misime.

Amesema yeyote atakayesalimisha silaha haramu ndani ya kipindi cha msamaha, hatoshtakiwa na wala hakutohitajika kutaja jina lake, wala kueleza alikuwa anatumia kwa shughuli gani silaha husika.

DCP Misime amesema baada ya kuisha kwa muda wa msamaha, jeshi hilo litaendesha msako nchi nzima na watakaokutwa nazo, watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

“Mwaka 2023 lilitolewa tangazo la msamaha kama hili na walioitikia wito walitumia fursa hiyo…silaha 337 na risasi 262 zilisalimishwa. Wapo ambao walipuuza na matokeo yake Jeshi la Polisi lilifanya msako nchi nzima na watuhumiwa 176 walikamatwa ambapo kati yao wanaume walikuwa 167 na wanawake 9. Silaha walizokamatwa nazo ni 195,” amesema.

Amesema katika msako huo, watuhumiwa saba walikamatwa kwa kukutwa na risasi 334 kinyume cha sheria; na baada ya kufikishwa mahakamani, wamefungwa jela na wengine kesi zao zinaendelea.

About The Author