WANAFUNZI 3,000 wanatarajiwa kujiunga na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kampasi ya Geita, iliyopo mtaa wa Mlimani, kata ya Muungano, wilayani Chato. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).
Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Josephat Lotto, amesema hayo wakati akitoa taarifa ya mradi kwa kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Godfrey Mnzava, aliyefika kukagua na kuweka jiwe la msingi kwenye kampasi hiyo.
Amesema lengo la kupokea wanafunzi katika kampasi hiyo, ni kusogeza huduma ya elimu ya vyuo vya kati kwa mkoa wa Geita na mikoa jirani, ili kutengeneza mazingira ya biashara na kujiajiri kwa vijana nchini.
Hata hivyo, ili kukamilisha ujenzi wa chuo hicho, Sh. 9.7 bilioni zinahitajika kwa ajili ya kujenga madarasa yenye thamani ya Sh. 476 milioni, jengo la utawala (Sh. 1.2 bilioni) na jengo la mihadhara (Sh. 797 milioni).
Baadhi ya majengo mengine na gharama zake kwenye mabano ni la chakula (Sh. 226.5 milioni), mabweni ya wanafunzi (Sh. 3.5 bilioni), nyumba za wafanyakazi (Sh. 548 milioni) na maktaba na tehama (Sh. 764 milioni).
“Ujenzi wa chuo hiki ulianza Januari 2021 kwa matayarisho ya awali, ujenzi wa majengo ya awamu ya kwanza ulianza Juni 2021, awamu ya pili ulianza Juni 2022,” amesema Prof. Lotto.
Mbunge wa jimbo la Chato (CCM), Dk. Medard Kalemani, amesema serikali imeshawalipa wananchi waliokuwa wanamiliki eneo la ekari 32, ambalo sasa litatumika kujenga chuo hicho.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava, ameagiza usimamizi uimarishwe ili mradi huo ukamilike kwa wakati kama ilivyopangwa.
Ukiwa wilayani Chato, Mwenge wa Uhuru utakagua, kuzindua, kutembelea na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mkuu wa wilaya ya Chato, Loys Peter, amesema Mwenge wa uhuru ndani ya wilaya hiyo utakimbizwa umbali wa kilometa 145 na kukagua miradi 10 yenye thamani ya Sh. 10.6 bilioni.
ZINAZOFANANA
Wanafunzi Tusiime waanza ziara nchini Uturuki
‘CODE LIKE A GIRL’ imewajengea uwezo wa Tehama wasichana Dodoma
Tanzania yaandika historia: Wanafunzi wa Arusha Science wapata ushindi wa kimataifa