October 16, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wanaanga waliokwama anga za juu kurejea duniani Februari 2025

 

CHOMBO cha SpaceX kilichotumwa kuwarudisha wanaanga wawili waliokuwa wamekwama kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS), kimetia nanga. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Hata hivyo, chombo hicho kinachoitwa Dragon, ambacho kimefanikiwa kutua salama jana saa 11:30 jioni, kitawarejesha duniani wana anga, Butch Wilmore na Suni Williams, Februari 2025.

Wawili hao walifika katika anga za juu wakiwa na chombo kipya cha Boeing ya Starliner Juni mwaka huu, kwa lengo la kukaa siku nane, lakini walilazimika kubaki kwenye anga hizo kwa sababu ya hitilafu iliyogunduliwa wakati wa safari.

Chombo hicho cha Dragon kiliinuliwa kutoka Cape Canaveral, Florida siku ya Jumamosi kikiwa na mwanaanga wa Nasa Nick Hague na mwanaanga wa Urusi, Alexander Gorbunov.

Hague, ambaye amefanya kazi hapo awali kwenye ISS, na Gorbunov, wataungana na wafanyakazi wa kituo cha anga za juu kabla ya kuwarudisha Wilmore na Williams duniani.

Safari ya Dragon kuelekea anga za mbali ilikuwa imepangwa kufanyika Alhamisi wiki iliyopita, lakini ilicheleweshwa kwa sababu ya kimbunga Helene, cha hivi karibuni, kilichosababisha uharibifu mkubwa katika eneo la Kusini-Mashariki mwa Marekani, ikiwa ni pamoja na Florida.

Picha kutoka ndani ya ISS zilionyesha Hague na Gorbunov wakitabasamu na kupiga picha na wafanyakazi wengine baada ya kuwasili.

Kwa taarifa hiyo ni kwamba safari ya siku nane ya wana anga hao waliokwama tangu Juni mwaka huu, imekuwa ya zaidi ya nusu mwaka hadi Februari mwakani.

About The Author