October 16, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Jaji Warioba: Sokoine alikubali kuulizwa maswali magumu, alikuwa mfuatiliaji

Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba

 

MAKAMU wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema hayati Edward Sokoine, alikuwa kiongozi aliyekubali kuhojiwa na kuhoji utendaji wa kila siku bila hofu, kwa nia ya kuwaletea wananchi maendeleo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ameyasema hayo wakati wa uzindzi wa kitabu cha Edward Sokoine: Maisha na Uongozi Wake, uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Septemba 30, 2024.

Amesema Sokoine alichukua wadhifa wa Waziri Mkuu akiwa na umri wa miaka 39, kwenye Baraza la Mawaziri lilikokuwa na mawaziri vijana wengi kuliko wazee.

Jaji Warioba amesema ilikuwa rahisi kwenda kwa Sokoine kuliko kwa Mwalimu Julius Nyerere.

“Uongozi wake ulikuwa ni jumuishi. Sokoine alikuwa anafuatilia kwa karibu sana utendaji wa serikali.

Alikuwa anauliza maswala mengi sana kuhusu utendaji na yeye alikubali awe anaulizwa maswali mengi. Kwa sababu alikuwa ni kijana mwenzetu, tulikuwa tumezoeana na hata alipokuwa Waziri Mkuu, tulindelea kuwa na uhusiano ule ule.”

“Kulikuwa na wakati kunakuwa na mjadala, anatu-challenge na sisi tulim-challenge, wakati mwingine tunatofautiana, mkija kumaliza tofauti zile, mnaendelea na kazi kama kawaida,” amesema.

Jaji Warioba amesema: “Tuliofanya naye kazi, alituimarisha sana, tuwe waaminifu kwa nchi yetu, kwa wananchi na viongozi. Alituimarisha tuwe waadilifu, nidhamu na wakati wote kwa Sokoine, focus (lengo), ilikuwa manufaa kwa wananchi. Kitabu hiki kwa haya yaliyomo, yatawasaidia sana viongozi vijana wa siku hizi, kuona jinsi Sokoine na hasa alivyosimamia utendaji wa serikali. Ni msaada mkubwa hasa kwa uongozi wa nchi hii.”

Amesema Sokoine alichukia rushwa na ufisadi kiasi kwamba alitunga sheria mahsusi kukabiliana na vitendo hivyo nchini.

Amesema Sokoine aliongoza Baraza la Mawaziri vijana, kukiwa na mabadiliko makubwa nchini, akisema ni wiki moja baada ya kuasisiwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wiki mbili baada ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Amesema mwaka mmoja baada ya Sokoine kuingia madarakani, Tanzania iliingia kwenye vita na Uganda, kumng’a Iddi Amini Dada na mwaka uliofuata, mafuta yalipanda bei kupita kiasi duniani.

Warioba Amesema aliporejea kwenye Uwaziri Mkuu kwa mara ya pili, Sokoine alitunga sheria ya kukabiliana na ufisadi, ambayo yeye (Warioba), alipinga baadhi ya vipengele na kutaka kujiuzulu Uwaziri wa Sheria.

Alisema alipinga vipengele vinne kikiwamo cha kesi za ufisadi kusikilizwa faragha, kuzuia dhamana kwa watuhumiwa, mahakama maalumu ya mafisadi na kufungua kesi kwa maneno ya kusikia.

Amesema alipinga vipengele hivyo kwa kuwa vilikuwa vilikuwa kinyume cha utu na haki za haki za binadamu na alitofautiana na wenzake 12.

Amesema baada ya hoja zake kukosa nguvu, aliamua kukaa pembeni, uamuzi uliopingwa na Sokoike kiasi cha kwenda kumshtaki Warioba kwa Mwalimu Nyerere Msasani.

Amesema Mwalimu Nyerere aliwasikiliza na kuwashauri kwenda kuondoa kipengele cha kesi kusikilizwa faragha na kufunguliwa kwa maneno ya kusikilizwa. “Tukatoka pale, Sokoine akaniambia hakuna mtu kuacha hapa.”

Amesema sheria hiyo ilipitishwa April 1983, ikatumika Mei na kisha Juni mwaka huo huo, ikarudishwa bungeni kufanyiwa marekebisho, baada ya operesheni ya kukabiliana na vitendo hivyo, kuumiza watu wasiokuwa na hatia.

“Ile operesheni ilimsikitisha sana. Wale viongozi aliowategemea, wakaanza kujitenga.”

About The Author