December 25, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Israel yazidisha mashambilizi, ikiapa kuiteketeza Hezbollah

 

WAZIRI wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant, amekutana na wanajeshi karibu na mpaka wa Lebanon na kuwaambia watawarudisha raia waliokimbia makazi yao kaskazini mwa Israel kwa ‘njia zetu zote.’ Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Amewaambia wanajeshi kuwa kuuawa kwa kiongozi wa Hezbollah wiki iliyopita, Sayyed Hassan Nasrallah, ‘ni hatua muhimu sana, lakini sio mwisho wa mapambano.’

Katika video fupi, anaonekana akiwaambia wanajeshi kwamba: “Tutatumia uwezo wote tulionao na ikiwa mtu hakuelewa nini maana ya uwezo wote – ni uwezo wote.”

“Kila kitu kinachohitajika kufanywa, kitafanyika na tutatumia nguvu zote kutoka angani, bahari na nchi kavu.”

Wakati Israel ikiweka kiapo hicho, Naibu kiongozi wa Hezbollah, Naim Qassem, amesema kundi hilo liko tayari kwa uvamizi wa ardhini.

Hiyo ni hotuba ya kwanza kutoka kwa ofisa wa ngazi za juu wa Hezbollah, tangu kuuawa kwa kiongozi wao wiki iliyopita.

Wachambuzi wa siasa za Mashariki ya Kati, wamesema Qassem ametuma ujumbe kwamba, licha ya mashambulizi makali kutoka Israel, yaliyoua viongozi waandamizi wa Hezbollah, kundi hilo litakuwa imara.

Kuhusu nani atachukua nafasi ya Nasrallah, amesema baraza la kundi hilo, litaamua hivi karibuni kwa kuwa makamanda wote na viongozi wa ngazi za juu walikuwa na manaibu ambao wanaweza kujaza pengo waliloacha.

Amesema Hezbollah inajua vita vyake na Israel vinaweza kuwa ndefu, lakini wanajiandaa kwa lolote.

“Tuko tayari kwa uvamizi wa ardhini, na tutaibuka washindi,” amesema.

Kwa upande mwingine, Israel imedai roketi 35 zimerushwa kutoka Lebanon kuelekea Kaskazini mwa Israel asubuhi ya leo.

Jeshi la Israel (IDF), limesema baadhi ya roketi hizo zilizuiliwa huku nyingine zikianguka katika maeneo ya wazi.

Nalo kundi la wapiganaji wa Kipalestina la Hamas, linasema kuwa kiongozi wake nchini Lebanon, Fateh Sherif Abu el-Amin, ameuawa pamoja na baadhi ya jamaa zake katika shambulio la anga la Israel, Kusini mwa Lebanon.

Hamas imesema kiongozi huyo aliuawa katika shambulio kwenye nyumba yake katika kambi ya Al-Bass, Kusini mwa Lebanon.

Shirika la habari la serikali la Lebanon liliripoti shambulio la anga dhidi ya kambi hiyo karibu na mji wa kusini wa Tiro.

Ingawa Hamas wako Gaza ambako Israel imekuwa ikipambana nao tangu mashambulizi ya Oktoba 7, mwaka jana, pia wapo nchini Lebanon.

Makundi ya Hamas na Hezbollah zote yanaungwa mkono na kufadhiliwa na Iran.

Wakati huo huo , Iran imesema ‘vitendo vya kihalifu’ vya Israel vitajibiwa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kanaani, amesema Iran haitaacha vitendo vyovyote vya uhalifu vya Israel bila majibu.

Katika mashambulizi ya Ijumaa, Jenerali mkuu katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, aliuawa mjini Beirut ambako pia aliuawa kiongozi wa Hezbollah.

Aidha, taarifa za leo Jumatatu, zinaeleza kuwa jeshi la Israel limemuua mkuu wa kitengo cha usalama wa kundi la Hezbollah, Nabil Kaouk, huku likizidisha mashambulizi katika maeneo ya Hezbollah mjini Bekaa.

Vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti kuwa leo tarehe 30 Septemba 2024, Jeshi la Israel limefanya mashambulizi mapya kadhaa kwenye ‘maeneo ya Hezbollah’ nchini Lebanon.

Jeshi hilo limedai kumuua Kaouk katika shambulio la anga lilifanyika juzi Jumamosi tarehe 28 Septemba 2024; na tayari Hezbollah imethibitisha kifo chake, na kumfanya kuwa kiongozi wa saba wa ngazi za juu wa kundi hilo kuuawa katika mashambulizi ya Israel katika muda wa zaidi ya wiki moja.

Israel inamtuhumu Kaouk kuhusika na mashambulizi ya kigaidi dhidi yake tangu alipojiunga na kundi hilo miaka ya 1980.

Katika taarifa yake, Jeshi la Israel limeapa kuendelea kuwaangamiza makamanda wa kundi la Hezbollah, baada ya kumuua Nasrallah huko Beirut, Lebanon, wiki iliyopita.

Katika shambulizi la Ijumaa iliyopita, Israel ilisema pia iliwaua viongozi wengine 20 muhimu katika kundi hilo linaloungwa mkono na Iran.

Miongoni mwa waliouawa ni jenerali mkuu katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, Abbas Nilforoushan, tukio lililoripotiwa na vyombo vya habari vya serikali ya Iran.

Maafisa wa Lebanon wamesema zaidi ya watu 100 wameuawa jana Jumapili, na kufanya idadi ya vifo ndani ya wiki mbili zilizopita kufikia 1,000.

Waziri Mkuu wa Lebanon, Najib Mikati, amesema mashambulizi ya anga ya Israel huenda yakawafanya watu wapatao milioni moja kuyahama makazi yao.

Katika hatua nyingine , kundi la wanamgambo wa Kipalestina, limesema leo kuwa viongozi wake watatu waliuawa katika shambulizi la Israel huko Beirut.

Chama cha Popular Front for the Liberation of Palestine (PFLP) kilisema viongozi hao watatu waliuawa katika shambulio lililolenga wilaya ya Kola ya Beirut.

PFLP ni kundi jingine la wanamgambo wanaoshiriki katika vita dhidi ya Israel.

Israel pia ililenga kundi jingine linaloungwa mkono na Iran, Houthi, nchini Yemen, ikidai kuwa walikuwa wakijibu mashambulizi ya kundi hilo dhidi yake.

Kuongezeka kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah na Houthi, Lebanon na Yemen, kumezusha hofu kwamba mapigano ya Mashariki ya Kati yanaweza kutoka nje ya udhibiti na kuteka Iran inayoyaunga mkono makundi hayo na Marekani, ambayo ni mshirika mkuu wa Israel.

About The Author

error: Content is protected !!