December 25, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Rais Samia atabiri makubwa Ruvuma akihitimisha ziara yake

Rais Samia Suluhu Hassan

 

RAIS Samia Suluhu Hassan, amehitimisha ziara yake mkoani Ruvuma, huku akijivunia ujenzi wa miradi ya maendeleo inayoendelea mkoani humo, itakavyowaondolea wananchi umaskini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Ruvuma … (endelea).

Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma, Rais Samia amesema kwenye wilaya zote alizopita ameona maendeleo makubwa.

Akianza na sekta ya kilimo, amesema serikali inakusudia kujenga maghala 28 ya kuhifadhia nafaka, kuongeza ruzuku ya pembejeo za kilimo, vikiwamo vifaa pamoja na kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani.

Amesema ujenzi wa maghala unatarajiwa kuongeza uwezo wa Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kununua na kuhifadhi nafaka hadi tani 28,000 mkoani Ruvuma.

“Kupitia NFRA, tumetengeneza mifumo itakayotuwezesha kununua tani 170,000 za mahindi zenye thamani ya Sh. 119 bilioni na hadi jana, wakala umeshanunua tani 63,467 kwa Sh. 44.43 bilioni,” amesema.

Kuhusu kuongeza ruzuku, Rais Samia amesema imeongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, ikiwamo kahawa, korosho, ufuta, mbaazi na soya; ambayo yatawaingizia wakulima fedha nyingi.

Amesema serikali imetoa ruzuku ya mbolea yenye thamani ya Sh. 83.5 bilioni ambayo imeongeza matumizi kutoka tani 32,139, mwaka juzi (2022) hadi tani 121,490 msimu ulioisha mwaka huu, ambalo ni ongezeko la matumizi ya mbolea kwa asilimia 283.

Alisema zuruku ya viuatilifu na mbolea kwa wakulima wa korosho, imeongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka tani 25,000 msimu wa 2021/22 hadi tani 21,109 msimu wa 2023/24.

Amesema lengo ni kufikia tani 55,730 msimu ujao na kwamba zao hilo limetengewa ruzuku ya pembejeo zenye thamani ya Sh. 46.8 bilioni.

Rais Samia, amesema ili kukifanya kilimo kiwe endelevu, serikali inaimarisha skimu za umwagiliaji ili mwaka 2030, kilimo hicho kifikie asilimia 50.

Amesema mkoani humo, miradi 33 ya umwagiliaji inaendelea na ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi, ukarabati, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika skimu, mabwawa na mabonde.

Amesema msimu uliopita, mazao ya yenye thamani ya Sh. 79.4 bilioni yaliuzwa na hivyo kuwaondolea wananchi umasikini.

Baadhi ya mazao na thamani ya mauzo yake kwenye mabano ni ufuta (Sh. 31.8 bilioni), mbaazi (Sh. 8.5 bilioni), soya (Sh. 4.1 bilioni) na kahawa (Sh. 16 bilioni).

“Huku ni kupunguza kwa kiasi kikubwa umasikini wa wananchi. Linaloendelea hivi sasa ni wananchi kuwa waangalifu kwenye matumizi ya fedha zote hizi ili waondokane na umasikini,” amesema.

Amesema stakabadhi ghalani ndio mfumo utakaoendelea kununua mazao nchini ili kuwahakikishia wakulima bei nzuri na kuweka takwimu sahihi za serikali kuhusu sekta ya kilimo.

Kwenye sekta ya elimu, amesema jitihada zitaendelea kufanyika katika kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari, kuhakikisha zinakuwa na vifaa vyote vya kufundishia na kujifunzia.

Akiwa mkoani humo, Rais Samia alizindua shule ya msingi ya mchepuo wa Kiingereza na sekondari maalumu ya wasichana.

Kwenye afya, amesema katika kipindi cha miaka mitatu serikali imepeleka Sh. 30.53 bilioni mkoani Ruvuma, ambazo zimejenga Zahanati 21, Vituo vya Afya 14, majengo ya dharura manne, chumba kimoja cha wagonjwa mahtuti, hospitali tano za wilaya na kukarabati wa hospitali mbili. Pia amesema katika kipindi hicho, serikali imepeleka magari 15 ya wagonjwa na saba ya usimamizi wa shughuli za afya.

“Upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitenganishi ni asilimia 65 mkoani Ruvuma. Tutaiwezesha MSD (Bohari ya Dawa), ili upatikanaji uongezeke zaidi,” amesema.

Kwenye sekta ya maji, alisema hivi sasa yanapatikana kwa asilimia 71 na kwamba miradi inayoendelea itakapokamilika, wananchi walio maeneo ya vijijini mkoani humo watapata maji kwa asilimia 80.3 na mijini asilimia 95.
Kwenye miundombinu, ameiagiza wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kukarabati barabara ya Songea-Njombe hadi Makambako, haraka iwezekanavyo.

“Tunataka kuijenga reli Mtwara hadi Ruvuma na itapita machimbo ya Liganga na Mchuchuma. Lengo ni kukuza ushoroba wa Mtwara,” amesema.

Kuhusu mawasiliano, alisema minara 26 inajengwa mkoani Ruvuma, ili kuimarisha mawasiliano ya simu mijini na vijijini na kuwawezesha wananchi kupata taarifa mbalimbali zikiwamo za masoko mapema.

Amewataka wananchi mkoani humo kujiandikisha kwenye daftari la kupiga kura na kukichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye chaguzi zijazo.

About The Author

error: Content is protected !!